Jeshi la Myanmar lashutumiwa kupanga mauaji ya Rohingya
19 Julai 2018Umoja wa Mataifa na Marekani zimeitaja kampeni hiyo kuwa safisha safisha ya kikabila, lakini serikali ya Myanmar inakanusha tuhuma hizo, ikisema ilikuwa inajibu mashambulizi yaliofanywa na wapiganaji wa Rohingya.
Shirika la kuteteta haki za binadamu la Fortify, katika ripoti yake iliotokana na uchunguzi wa miezi kadhaa nchini Myanmar na Bangladesh na mahojiano na mamia ya waathirika pamoja na maafisa wa serikali, limegundua kuwa vikosi vya usalama viliwaondolea Warohingya uwezo wa kujilinda kwa kuwanyanganya zana zote za ncha kali, na kutoa mafunzo kwa jamii zisizo za Rohingya kupigana.
Ripoti hiyo inabainisha kuwa jeshi la Myanmar pia lilizuwia chakula na msaada wa kiutu kwa Warohingya ili kuwadhoofisha kuelekea ukandamizaji huo wa mwaka 2017. Ripoti hiyo inahitimisha kuwa serikali ilifanya maandalizi mapana na kiutaratibu dhidi ya Warohingya.
Ripoti hiyo inasema hata mashambulizi mabaya yaliofanywa Agosti 25, 2017 na wapiganaji wa kundi la Rohingya la Jeshi la ukombozi la Arakan, ambayo Myanmar iliyataja kama sababu ya operesheni yake, yalikuwa ni tukio dogo tu kuliko ilivyoaminika awali, na kwamba mipango ya ukandamizaji tayari ilikuwa inaendelea.
Mauaji ya halaiki
Mwasisi mwenza wa shirika la Fortify Matthew Smith, aliwaambia waandishi habari wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo mjini Bangkok, kwamba vikosi vya usalama viliwafanya Waislami wa hamii ya Rohingya katika jimbo la Rakhine kuwa dhaifu na kuwaweka katika hatari ya kushambuliwa.
"Jeshi la Myanmar linataka kuiaminisha dunia kwamba lilikuwa linapambana dhidi ya ugaidi katika jimbo la Rakhine na kwamba huu ulikuwa uitikiaji wa papo kwa papo. Lakini tuna ushahidi wa namna jeshi lilifanya maandalizi ya ukandamizaji huu miezi kadhaa kabla ya kuanza kwa operesheni ya Agosti 25, 2017.
Tunatumai kwamba ripoti hii itachochea kuchukuliwa kwa hatua za maana, na sasa hivi baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linapaswa kuzishinikiza nchi nyingine kwenye baraza kuhakikisha kwamba kesi hii inahamishiwa katika mahakama ya ICC haraka iwezekanavyo."
Watu wasio na utaifa
Warohingya wameishi kwa muda mrefu katika jimbo la Rakhine lakini wanachukuliwa kama watu wa nje na Myanmar yenye wafuasi wengi wa madhhabu ya Budha, baada ya miaka kadhaa ya propaganda za kuwatweza kutoka kwa tawala za taifa hilo. Fortify pia imewataja maafisa 22 wa jeshi na polisi kuwa wanaohusika na ukandamizaji huo, akiwemo mkuu wa majeshi Min Aung Haling.
Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Myanmar Yanghee Lee alionya mwezi uliopita kwamba nafasi ya kuwafikisha majenerali hao mbele ya mahakama mjini The Hague ni finyu, wakati ambapo taifa hilo linakingiwa kifua na washirika wenye nguvu ambao hata hivyo hakuwataja. Wanachama wa kudumu wa baraza la usalama Urusi na China waliiunga mkono Myanamar huko nyuma na kuitetea dhidi ya kuchunguzwa zaidi.
Ripoti hiyo pia imewashtumu wapiganaji wa Rohigya kwa kuwauwa raia kwa madai kwamba walikuwa watoa habari wa serikali.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape,afpe
Mhariri: Josephat Charo