Jeshi la Nigeria lakataa kutwaa madaraka
4 Mei 2021Jeshi la Nigeria limepuuza mapendekezo ya kulitaka lichukue madaraka yanayoshikiliwa na rais Mohamadu Buhari ambaye anazidi kukabiliwa na shinikizo kuhusiana na hali mbaya ya ukosefu wa usalama nchini humo.
Sio mara ya kwanza jeshi la ulinzi la Nigeria kutoa taarifa ya kumuunga mkono Buhari lakini taarifa ya karibuni imekuwa baada ya wiki kadhaa za kusikika kauli za kumkosoa kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 78 aliyewahi kuwa jenerali wa jeshi,kutokana na kushindwa kwake kuutatua mgogoro huo wa ukosefu wa usalama.
Kuanzia suala la uasi wa kundi la wapiganaji wa jihad huko kaskazini Mashariki hadi kwenye mapigano baina ya wakulima na wafugaji kwenye eneo la kati mwa nchi,matukio ya magenge ya majambazi huko Kaskazini Magharibi na mvutano wa wanaotaka kujitenga,Kusini Mashariki,jeshi la rais Buhari linaonesha kuwa katika hali ya kupambana kuzuia ukosefu wa usalama.
Msimamo wa jeshi
Siku ya Jumatatu jeshi hilo lilitowa taarifa kupitia taarifa msemaji wake Onyema Nwachukwu, likisema litaendelea kuiunga mkono kikamilifu serikali na kubakia kuwa chombo kisichojiingiza kwenye siasa na kuilinda demokrasia ya Nigeria.
Jeshi lilitia mkazo kwamba litailinda katiba ya nchi. Yote haya yamejitokeza baada ya wiki iliyopita wabunge kutoa mwito wa kutaka rais Buhari atangaze hali ya hatari nchi nzima baada ya kushuhudiwa mwezi mzima wa mashambulizi ya takriban kila siku,utekaji nyara na mauaji katika nchi hiyo yenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika.
Taarifa ya jeshi hasa ilikuwa ikilenga kujibu matamshi ya mwanasheria maarufu nchini humo Robert Clerk,aliyesema nchi iko ukingoni kuporomoka na akatoa pendekezo la kutaka uongozi wa kisiasa uliachie jeshi madaraka ili vikosi vya usalama viweze kujipanga upya.
Shinikizo
Na hata watu wengine mashuhuri nchi humo kama Bukola Saraki na mshindi ya tuzo ya Nobel ya fasihi Wole Soyinka walimtolea mwito Buhari atafute usaidizi kutoka nje au ajiuzulu madarakani.Wiki iliyopita Buhari alikutana na wakuu wake wa usalama na kwa mara nyingine leo Jumanne kujadili juu ya machafuko yanayoikabili nchi.
Jeshi kwa upande mwingine limezungumzia matarajio kwamba changamoto za kiusalama zinazoikabili Nigeria kwa sasa sio za kutoweza kudhibitiwa.Kumbuka Nigeria ilirudi kwenye demokrasia mnamo mwaka 1999 baada ya kukaa miaka takriban 16 chini ya utawala wa kijeshi.
Buhari binafsi aliwahi kuwa mtawala wa kijeshi miaka ya 1980 na alichaguliwa kwa mara ya kwanza kwa njia za kdemokrasia mnamo mwaka 2015 na miaka minne baadae akachaguliwa tena kwa ahadi kwamba ataumaliza uasi wa wanamgambo wa Boko Haram Kaskazini Mashariki. Lakini kinyume chake uasi wa wanamgambo hao wa itikadi kali umezidi kuongezeka kukiweko makundi mawili yaliyogawika,Boko Haram na lile linalojiita dola la kiislamu la mkoa wa Afrika Magharibi ISWAP, kwa ufupi likiwa ndilo lenye nguvu kubwa.
Na kama haitoshi machafuko yameenea hadi kwenye nchi jirani za Chad,Niger na Cameroon na kuchochea kuundwa muungano wa jeshi la kikanda kupambana na wanamgambo hao.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri: Gakuba, Daniel