1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Nigeria lawaonya vijana juu ya maandamano ya vurugu

26 Julai 2024

Rais wa Nigeria Bola Tinubu na jeshi la nchi hiyo wameonya juu ya kufanyika maandamano ya vurugu kama yaliyotokea Kenya na ambayo yamepangwa kufanyika wiki ijayo nchini humo kulalamikia kupanda kwa gharama ya maisha.

Nigeria | Bola Tinubu
Rais wa Nigeria Bola Ahmed Tinubu Picha: Sunday Aghaeze/Nigeria State House via AP/picture alliance

Jeshi la Nigeria limesema limejiandaa kukabiliana na uvunjaji wa sheria. Rais Tinubu amesema katika taarifa kuwa hawaogopi maandamano bali wasiwasi wao ni kuhusu usalama wa raia na uharibifu ambao huenda ukatokea.

Kiongozi huyo ametoa mwito kwa raia wa nchi hiyo kuwa waangalifu na kuonya juu ya kuigeuza Nigeria kama Sudan, akiashiria vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miezi 15 katika nchi hiyo ya kaskazini mashariki mwa Afrika.

Maafisa wa serikali, vikosi vya usalama na magavana nchini Nigeria wamewarai vijana kujiepusha na maandamano. Baadhi ya viongozi wameshtumu waandaaji wa maandamano hayo kwa uhaini na kuwa na nia ya kuliyumbisha taifa.

Nigeria kuendelea na mageuzi ya kiuchumi

Kenya ilikumbwa na maandamano makubwa yaliyoilazimu serikali kutupilia mbali mswada tata wa fedha uliotoa mapendekezo ya kuongeza ushuru. Mageuzi ya kiuchumi ya Nigeria yameshuhudia ongezeko la asilimia 40 ya mfumuko wa bei ya vyakula.

Kumetolewa miito katika mitandao ya kijamii kwa Wanaigeria kufanya maandamano kulalamikia kupanda kwa gharama ya maisha kuanzia Agosti mosi. Hata hivyo haijabainika ni kina nani hasa wanaochochea maandamano hayo au hata iwapo watu watajitokeza barabarani hasa wakati huu ambapo raia wengi wa Nigeria wana hofu juu ya kupoteza kazi zao au uwoga wa kukamatwa.
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW