1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Nigeria lashutumiwa na Amnesty International

Admin.WagnerD4 Juni 2015

Jeshi la Nigeria limeshutumiwa na Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International, kwa kufanya mauwaji ya zaidi ya watu 8,000 katika kempeni yake dhidi ya kundi la kigaidi la Boko Haram.

Symbolbild Nigeria Armee
Picha: picture alliance/AP Photo/Gambrell

Shirika hilo la kimataifa la kutetea haki za binaadamu limesema jana kuwa kuna ushahidi wa kutosha wa kufungua kesi katika Mahakama ya kimataifa inayoshughulikia uhalifu ya ICC, dhidi ya maafisa waandamizi wa jeshi la Nigeria kwa uhalifu wa kivita walioufanya wakiwa katika mchakato wa kupambana na kundi la kigaidi la Boko Haram. Hata hivyo jeshi la Nigeria limepinga madai hayo.

Shirika hilo la kimataifa limeandaa ripoti maalimu ya kurasa 133 ambayo inadai kuwa zaidi ya watu 8,000 walifariki wakiwa kizuizini chini ya jeshi la Nigeria, wakati wa kampeni yake ya kupambana na kundi hilo la Boko Haram.

"Amnesty International inaamini kwamba sababu kuu za vifo kwa waliokuwa kizuizini zilikuwa ni pamoja na njaa, ukosefu wa hewa, msongamano mkubwa ambao ulisababisha kuenea kwa magonjwa, mateso, ukosefu wa matibabu na matumizi ya madawa ya mafusho katika seli zisizo na njia za kupitisha hewa. Hitimisho hili linatokana na ushahidi wa wataalamu, uchambuzi wa ushahidi wa video na picha na habari zilizomo katika ripoti za vyombo vya habari." alisema Mkurugenzi wa Afrika, juu ya utafiti na utetezi wa shirika la Amnesty International, Netsanet Belay akizungumzia juu ya baadhi ya mateso na unyanyasaji waliofanyiwa watu hao na jeshi la Nigeria.

Netsanet Belay wa shirika la Amnesty InternationalPicha: Karen Hatch Photography

Ahadi ya rais Buhari na jeshi kujitetea

Rais mpya wa Nigeria Muhammadu Buhari ameahidi kushughulikia madai hayo, ambayo yanawalenga maafisa waandamizi watano wa jeshi madai ambayo yanatokana na nyaraka zilizovuja za wizara ya ulinzi pamoja na mamia ya mahojianoa na waathirika, mashahidi pamoja na baadhi ya wanajeshi yaliyofanywa na shirika hilo.

"Utawala mpya utafanya kila liwezalo kuukuza utawala wa sheria na kuhakikisha unashughulikia visa vyote vinavyohusika na unyanyasaji wa haki za binadaamu," alisema Buhari.

Katibu Mkuu wa Shirika la Amnesty International Salil Shetty amesema unyanyasaji uliofanywa na jeshi la Nigeria ni wa kukirihisha, lakini jeshi hilo limekana madai hayo na kusema kuwa iliandikwa ili kuchafua jina na hadhi ya jeshi hilo.

"Maafisa ambao wametajwa katika ripoti hio, hawana sababu zozote za kufanya mtendo yaliyodaiwa dhidi yao. Ni jambo la kusikitisha kuona kuwa shirika la Amnesty International, limekusanya majina ya maafisa hawa kwa mipango tu ya kutaka kuharibu majina yao pamoja na jina la jeshi la Nigeria," alidai msemaji mkuu wa wizara ya ulinzi ya Nigeria Chris Olukolade

Aliongeza kwa kusema jeshi la Nigeria linapinga sana unyanyasaji wa haki za kibinaadami, na atakaepatikana na hatia ya visa hivyo atawajibishwa kwa adhabu ipasayo.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/AFPE/RTRE

Mhariri:Iddi Ssessanga