1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Pakistan laendesha oparesheni kali dhihi ya wanamgambo wa Taliban.

Jason Nyakundi8 Mei 2009

Maelfu ya watu waendelea kulikimbia bonde la Swat.

Wanamgambo wa Taliban.Picha: picture-alliance/dpa

Huku mapambano yakiendelea kuchacha kati ya wanamgambo wa Taliban na wanajeshi wa Pakistan na kuvishinda vita dhidi ya wanamgambo, jeshi la Pakistan litahitajika kuzuia uharibifu mkubwa na pia kuwahudumia raia walioyatoroka mapigano hayo.

Wanamgambo wa Taliban wamedhibiti zaidi ya nusu ya eneo la kaskazini magharibi mwa Pakistan hata baada ya oparesheni zilizofanywa na jeshi la Pakistan kwa muda wa mika miwili iliyopita na baada ya mapigano yaliyodumu kwa miaka sita.

Jeshi la Pakistan limepoteza zaidi ya wanajeshi elfu mbili tangu mwaka 2002 na linadai kuwaua maelfu ya wanamgambo, lakini hata hivyo bado wanamgambo wa Taliban wanaendelea kuchukua maeneo zaidi.

Hii leo wanajeshi wa Pakistan waliwaua zaidi ya wanamgambo 30 siku moja tu baada ya waziri mkuu wa Pakistan Yusuf Raza Gilani kutangaza oparesheni kali katika bonde la Swat

Jeshi lilitumia ndege za kijeshi pamoja na silaha zingine nzito kushambulia maficho ya wanamgambo wa Taliban huku mamia ya watu wakihamia maeneo salama.

Vita hivyo vinatajwa kuwa hatari na vigumu kwa wanajeshi kupigana na wanamgambo wa Taliban katika eneo hilo lililo na milima na ni vigumu kisiasa kupigana vita na waislamu wenzao.

Hivi sasa Pakistan ina karibu wanajeshi laki saba na kawaida, inaiona India kama adui wake mkubwa. Jeshi linasema kuwa wanajeshi laki moja kwa sasa wamewekwa katika maeneo ya magharibi karibu na mpaka na Afghanistan.

Hata hivyo haijabainika ikiwa idadi kubwa ya wanajeshi walio katika mikoa ya Punjap na Sindh karibu na mpaka na India watapelekwa vitani hadi kuafikiwa kile rais wa Pakistan Asif Ali Zardari amekitaja kuwa kurejea kwa hali ya kawaida.

Maelfu ya raia wameyakimbia maeneo ya mapigano hasa katika wilaya za Buner, Lower Dir na Swat, hatua ambayo itazuia vifo vya raia zaidi.

Wanajeshi wa Pakistan wakielekea katika bonde la Swat.Picha: AP

Jeshi la Pakistan lina uwezo wa kumaliza uasi huo kwa muda wa wiki chache, lakini serikali kwa njia ya kidemokrasia itahitajika kuwa na mikakati ya kuhakikisha kuwa inachukua udhibiti wa kudumu wa hali hii.

Ndege za kijeshi, vifaru pamoja na silaha nyingine nzito zimewekwa tayari kwa vita hivyo vilivyoanza mwishoni mwa mwezi uliopita wa Aprili, baada ya wanamgambo wa Taliban kusonga mbele hadi wilaya ya Buner kutoka bonde la Swat, hata baada ya kutiwa saini makubaliano ya amani mwezi Februari mwaka huu.

Jeshi la Pakistan linasema kuwa hadi wapiganaji elfu tano wa Taliban wako katika Bonde la Swat wakiwemo kutoka kabila la Pashtun na makundi kutoka madhehebu ya Sunni, ambao wamekuwa wakipigania uhuru katika eneo la Kashmir linalodhibitiwa na India.

Wadadisi wanasema kuwa jeshi la Pakistan halina vifaa muhimu ikiwemo miwani ya kuonea wakati wa usiku pamoja na mitambo ya kuvuruga mawasiliano ya wanamgambo hao.

Inasemekana kuwa huenda jeshi la Pakistan likachukua muda wa karibu miezi miwili kumaliza oparesheni hiyo, lakini serikali ni lazima tena kwa haraka pia ijaribu kukabiliana na uasi kutoka kwa wale walioyakimbia mapigano hayo.

Kuna hofu kuwa huenda oparesheni hiyo ikasababisha uharibifu mkubwa. Pia watu wana hofu kuwa wakati jeshi litakapoondoka wanamgambo wa Taliban tena watarejea.

Mwandishi : Jason Nyakundi/AFP

Mhariri : Josephat Charo




Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW