Jeshi la polisi Tanzania laonya dhidi ya maandamano
2 Agosti 2021Akizungumza na waandishi wa habari mapema Jumatatu mkuu wa jeshi la polisi Simon Sirro amesema jeshi hilo lilifanikiwa kuzima majaribio kadhaa ya uhalifu katika kipindi cha uchaguzi na waliohusika walitaka kutumia sura ya maandamano ya kupinga kufanyika kwa zoezi hilo ili kutekeleza uhalifu waliodhamiria ikiwemo kuchoma vituo vya mafuta na hata njama za kufanya mauaji kwa baadhi ya viongozi.
"Jeshi la polisi linatoa onyo kwa mtu au kikundi cha watu kitakachojaribu kuhamasisha mikusanyiko isiyo rasmi au kuandamana au namna yoyote ile kutoa shinikizo lolote,"amesema.
Sirro ambae amekuwa akishutumiwa vikali na wafuasi wa chama hicho katika mitandao ya kijamii kuwa anatumika kufifisha democrasia ya taifa hilo la Afrika Mashariki ameonya vikali mtu ama kikundi cha watu watakaohamasisha mikusanyiko isio halali, jeshi la polisi halita sita kumchukulia hatua za kisheria.
"Jeshi la polisi halitegemei mtu au kikundi cha watu kwa namna yoyote kutoa shinikizo kwa mamlaka ya mahakama au kwa mtuhumiwa Freeman Mbowe aachiwe au kupewa dhamana,"amesema Sirro.
Soma pia: Polisi Tanzania: Wapinzani mlioko uhamishoni rudini nyumbani
Sirro amewataka viongozi wa dini na taasisi nyingine ziache kusema Mbowe anaaonewa na badaala yake wasubiri mahakama iamue.
"Jambo usilolijua ni kama usiku wa giza, yeye kapelekwa mahakamani tusubiri maamuzi, mikoa iliyojipanga kufanya maandamano ni kuvunja sheria."
Chadema yasisitiza ina haki ya kufuatilia kesi ya Mbowe
Kufuatia hatua hiyo Chadema imesisitiza kwamba inayo haki ya kisheria kufuatilia mwenendo wa kesi ya mwenyekiti wao Freeman Mbowe, hivyo jeshi la polisi halina mamalaka ya kuwazuia kufika mahakamani na kitendo cha mkuu wa jeshi la polisi kuzuia ni kuingilia uhuru wa mahakama.
Maamuzi ya Chadema ya kuwahusisha wananchama na wafuasi wake katika shauri la mwenyekiti Mbowe lilitokana na maamuzi ya kikao cha dharura cha kamati kilichoketi kwa siku tatu mfululizo chini ya makamu mwenyekiti Bara Tundu Lisu mnamo siku moja baada ya kukamatwa kwa mwenyekiti wao.