Maefu ya raia walikimbia jeshi la serikali ya Cameroon
8 Desemba 2017Maelfu wako mbioni baada ya Rais Paul Biya kutangaza vita dhidi ya wanaotaka kujitenga. Wakati huo huo Nigeria imetoa wito wa kusitisha vurugu hizo na kusema haiunga mkono kabisa kugawanyika kwa Cameroon.
Barabara mpya ya Kumba-Mamfe katika eneo la Kusini Magharibi mwa Cameroon, iliyojengwa ili kuboresha usafiri na biashara, imekuwa tupu. Ni njia ambayo inaruhusu biashara kustawi kati ya mataifa ya Nigeria na Cameroon.
Lakini mfanyabiashara mwenye umri wa miaka 32, Ethel Takem, aliiambia DW kuwa yeye na wenzake walilazimika kusimamisha biashara zao wakati Rais Biya alipotangaza vita dhidi ya wanaotaka kujitenga mwishoni mwa juma lililopita: "Idadi ya vituo vingi vya ukaguzi ni jambo linalosumbua," alisema Takem.
Alifananisha wanajeshi wa rais na simba wenye njaa kali walioachiliwa huru kwenye kundi la watu wasio na kinga au hatia. "Wale ambao wanataka kuuwawa wanaweza kusafiri. Bado nina maisha yangu baadae, hivyo siwezi kuhama," alisema.
Hali pia ni ya wasiwasi katika miji ya Mamfe na Eyumojock, ambako wanajeshi na polisi wapatao sita waliuawa wiki iliyopita.
Mamfe ni mji wa makaazi ya Julius Ayuk Tabe, mtu anayejiita rais wa kwanza wa Ambazonia.
Ambazonia ni jina ambalo wanaotaka kujitenga wanaliita eneo hilo linalozungumza Kiingereza nchini Cameroon ambalo wanatarajia kuligeuza na kuwa nchi huru.
Serikali ya Cameroon inasisitiza kuwa wapiganaji wanaotaka kujitenga wanapewa mafunzo katika kanda hiyo na mpaka wa nchi jirani ya Nigeria.
Kwa mujibu wa mkaazi wa Mamfe, Peter Ayuk, vijana wengi wamekimbilia msituni kulikimbia jeshi.
"Kijiji cha rais wa sasa kimechomwa moto, wanajeshi wanazichoma nyumba. Vijana wote wako misituni," alisema.
Ukiukwaji wa haki za binaadamu
Ayuk aliiambia DW kuwa watu wengi wamepoteana na ndugu zao, ikiwa ni pamoja naye: anasema hajawaona wazazi wake wote wawili tangu zilipoanza harakati za kuwafurusha.Kijana huyo anasema kila mahala kuna wanajeshi katika eneo hilo huku akiongeza kusema kwamba wavulana wadogo wanauwawa na wengine wakikamatwa na hiyo ndiyo sababu kila mmoja anakimbilia msituni.
Nyeke George Likiye, mwanachama wa jumuiya ya kiraia kaskazini-magharibi mwa Cameroon, anasema aliiandikia barua serikali kulalamika kuhusu wanajeshi hao wa ziada.akisema kwamba kuna ukamataji wa kiholela unaofanywa na wanajeshi hao pamoja na watu kupigwa na kuteswa.
Lakini generali Melingui Noma, mmoja wa maafisa wa kijeshi wa ngazi za juu wa Cameroon, amekanusha madai hayo na kupinga tuhuma kwamba kuna ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa na wanajeshi.
akisema jeshi liko huko kulinda wananchi: Tukinukuu maneno ya jenerali huyo amesema "Tunajua kwamba ikiwa tunataka kushinda mgogoro huu tunapaswa kuhakikisha kuwa watu wako pamoja na sisi. Je, unawezaje kwenda kuwadhalilisha na kuwasumbua watu ambao unataka wakupe taarifa muhimu? Ikiwa hawawezi kutupa taarifa sahihi, ikiwa hawawezi kutuambia ukweli juu ya kinachotokea uwanjani, utaona kuwa idadi ya watu itageuka na kufuata yale makundi yanayotaka kujitenga."
Mazungumzo sio chaguo
Shule zimefungwa katika eneo linalozungumza Kiingereza - kaskazini magharibi na kusini-magharibi tangu Novemba mwaka jana, wakati wanasheria na walimu walipoitisha mgomo kuzuia kile wanachoamini ni matumizi makubwa ya lugha ya Kifaransa.
Vurugu zilianza wakati wanaotaka kujitenga walipojiunga nao na kuanza kuitisha uhuru kamili.
Mnamo Oktoba 1, walitangaza kile walichokiita uhuru wa Jamhuri ya Ambazonia na kuwataka wanajeshi kujisalimisha na kujiunga nao au kuondoka kwenye eneo lao.
Hadi sasa, wameua wanajeshi takribani 11 na polisi.
Rais Paul Biya hajawahi kulegeza kamba kuhusu uamuzi wake wa kupinga azimio la uhuru wa eneo hilo na amekataa kujadiliana.
Makundi yanayotaka kujitenga yamesema kwenye mitandao ya kijamii kwamba wataingia tu katika mazungumzo na serikali kwa masharti ya kutaka kujitenga.
Wakati haya yakijiri, Nigeria imetoa wito wa kumalizika kwa ghasia zinazoendelea nchini Cameron na kusema haiungi mkono kabisa kujitenga bali inaunga mkono kurudi kwa amani nchini humo.
Mwandishi: Fathiya Omar/DW/Moki Kindzeka/AFPE
Mhariri: Yusuf Saumu