1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Sudan ladai kuzuia shambulio la RSF

26 Novemba 2025

Majeshi ya serikali ya Sudan yamedai kuwa yamezuia jaribio la wapiganaji wa RSF kufanya mashambulizi licha ya kundi hilo kutangaza kusitisha mapigano siku ya Jumatatu.

Mkuu wa jeshi Sudan Abdel Fattah al-Burhan
Mkuu wa jeshi Sudan Abdel Fattah al-BurhanPicha: Stringer/Anadolu Agency/IMAGO

Wakati huo huo, Mshauri wa Trump anasema hakuna hata moja kati ya makundiyanayopigana nchini Sudan ambayo yamekubali mpango wa kusitisha mapigano.

Jeshi la Sudan limesema kuwa lilizuia uvamizi wa wapiganaji wa RSF siku ya Jumanne kwenye mji wa kimkakati wa Babanusa magharibi mwa Kordofan ambao wa sasa ndiyo ngome yao kuu kanda hiyo.

Babanusa ndiyo njia muhimu inayounganisha jiji la Khartoum kupitia Kordofan kuelekea Darfur ambako mwezi uliopita majeshi ya serikali yalipoteza udhibiti wa mji wa El Fasher.

Pendekezo la amani lakataliwa

Kutokana na jaribio hilo la uvamizi wa RSF, Sudan inasema kuwa wapiganaji hao hawana nia ya kusitisha vita na kwa hiyo mpango husika hautazaa matunda yoyote kwani unaashiria hila za RSF pamoja na Umoja wa Falme za Kiarabu kuutumia kupotosha matarajio ya mataifa mengine.

Mkuu wa wanamgambo wa RSF Mohammed Hamdan Daglo (katikati)Picha: Mahmoud Hjaj/AP Photo

Mjumbe maalum wa Marekani kwa masuala ya Afrika na mataifa ya Kiarabu, Massad Boulos amefahamisha kuwa licha ya jopo la wajumbe kutoka Marekani, Saudia, Umoja wa Famle za Kiarabu na Misri kujitokeza na mpango wa kusitisha vita, yumkini pande zote mbili katika mzozo huo zimekataa kuukubali.

Hali hii inazidisha wasiwasi kwamba mapigano yataendelea na raia wa Sudan kuzidi kuuawa na kuteseka. Hata hivyo, ameendelea kuzihimiza pande zote mbili kuzingatia umuhimu wa mpango huo bila kuweka masharti yoyote.

''Sio Jeshi la Sudan wala RSF waliokubali rasmi mpango huu muhimu wa kusitisha mapigano. Jana tulipokea maamuzi ya RSF kusitisha mapigano. Hatutarajii tu kutoshuhudia utekelezaji huo kutoka pande zote mbili, lakini pia wakubali misaada ya kibinadamu kufikishwa kwa wahanga bila kuweka masharti ya kisiasa wala kijeshi ili kuepusha maafa zaidi. Sisi pamoja na washirika wetu wa kimataifa tuko tayari kuunga mkono utelekezaji wa mpango huo na pia kutoa misaada ya kibinadamu,'' alisema Boulos.

Wito huu umetolewa saa chache baada ya kamanda wa RSF Mohamed Hamdan Daglo kutangaza kuwa upande wake wangesitisha mapigano kwa miezi mitatu. Lakini muda mfupi baadaye majeshi ya serikali yakatangaza kuwa yamezima jaribio la uvamizi kwa ngome yao muhimu kusini mwa nchi hiyo.

Mpango "mbaya zaidi" wa amani

Mpango wa kusitisha vita ulioandaliwa mwezi Septemba ukiratibiwa na Marekani ulipendekeza kuwepo na kipindi cha miezi mitatu kuwezesha misaada ya kibinadamu kuwafika raia. Hatua ambayo inapendekezwa kufuatwa ni kukomesha kabisa mapigano na kuwepo ya kipindi cha miezi tisa ya mpito ili kuwezesha utawala wa kiraia.

Suluhisho la mzozo wa Sudan liko wapi?

13:42

This browser does not support the video element.

Lakini Mkuu wa Jeshi la Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan ameupinga mpango huo ambao ameutaja kuwa ''mbaya zaidi'' uliopendekezwa na lengo ni kutanguliza maslahi ya Umoja wa Falme za Kiarabu nchi ambayo inatajwa kuchochea mzozo huo kwa kutoa ufadhili kwa RSF.

Katika mkutano wake na waandishi habari pamoja na mshauri wa kidiplomasia wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Anwar Gargash, Boulos amesema ukosoaji wa Al- Burhan unatokana na taarifa potofu.

Gargash mwenyewe amesema kuwa madai ya Al- Burhan pamoja na kampeni za kupotosha havitadhoofisha uhusika wa nchi yake katika kusaka amani ya Sudan.