1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Jeshi la Sudan lafuta uwezekano wa kusitishwa mapigano

11 Machi 2024

Jenerali mkuu wa jeshi la Sudan amesema hakutakuwa na makubaliano ya usitishaji mapigano wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan hadi pale wanamgambo wa RSF watakapoondoka kwenye makazi na maeneo ya raia.

RSF wakipiga doria katika mji mkuu Khartoum, Sudan.
Wanamgambo wa RSF wakiwa katika mji mkuu Khartoum.Picha: Hussein Malla/AP/picture alliance

Kauli ya Yasser al-Atta, naibu kamanda wa jeshi, inajiri baada ya jeshi kudai kupiga hatua katika mji wa Omdurman, pamoja na wito wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wa usitishwaji mapigano wakati huu wa Ramadhan.

Soma pia: Wanamgambo wa RSF watamani kusitishwa mapigano wakati wa mfungo

Taarifa ya Atta, iliyotolewa kupitia mtandao wa Telegram ilisema hakuwezi kuwa na usitishaji vita wakati wa Ramadhani hadi pale kundi la wanamgambo la  RSF litakapotimiza ahadi waliyoitoa mwezi Mei mwaka jana wakati wa mazungumzo ya upatanishi yaliyosimamiwa na Saudi Arabia na Marekani mjini Jeddah ya kujiondoa kutoka kwenye  maeneo ya raia.

Aidha taarifa hiyo ilisisitiza, hakutakuwa na nafasi au jukumu lolote kwa kiongozi wa RSF Mohamed Hamdan Dagalo, au familia yake, katika mustakabali wa kisiasa au kijeshi wa Sudan.

Nia njema wakati wa Ramadhan

Wanamgambo wa kikosi cha RSF kinachoongozwa na Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo.Picha: Hussein Malla/AP Photo/picture alliance

Kikosi cha RSF kimejibu na kusema kimekaribisha wito wa Umoja wa Mataifa wa kusitisha mapigano.

RSF pia imedai jeshi limekataa ombi lake la kuwakabidhi wafungwa 537 wa vita, kama ishara ya nia njema wakati wa Ramadhan kupitia Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC).

Hata hivyo jeshi limekanusha madai hayo na kusema halijapokea mawasiliano yoyote kutoka kwa kamati ya ICRC na kuongezea kusema kuwa madai ya RSF ni ya "uongo".

Huku haya yakijiri wakaazi katika maeneo ya Omdurman wilaya ya Wad Nubawi ambayo sasa yako chini ya udhibiti wa jeshi wangependa kusaidia kurejesha hali ya utulivu na kurekebisha uharibifu mkubwa uliosababishwa na vita.

Mohamed Abdel Rahman mmoja wa wakaazi wa Wad Nubawi anasema:

"Tunaiomba serikali itupe fursa, sisi vijana wa Wad Nubawi, kufanya matengenezo, kurudisha mandhari nzuri ya ujirani wetu. Ili kurudisha huduma, tunataka kufanya kazi kama vijana na vyombo rasmi ili kurudisha familia zetu, na tunatumai kuanza kufunga kwa mwezi wa Ramadhan majumbani mwetu."

Umoja wa Mataifa umesema takriban watu milioni 25 ambayo ni nusu ya idadi jumla ya watu wa Sudan wanahitaji misaada, huku wengine milioni 8 wameyakimbia makazi yao wakati njaa ikiendelea kuongezeka.

Soma pia: WFP: Sudan kuwa "janga kubwa zaidi la njaa duniani"

Washington inazituhumu pande zote mbili zinazopigana kufanya uhalifu wa kivita.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW