1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Sudan lajipanga kukabiliana na maandamano

17 Julai 2022

Vikosi vya usalama vimeshika doria katika mji mkuu Khartoum, kabla ya maandamano makubwa yaliyopangwa na makundi yanayounga mkono demokrasia dhidi ya kiongozi wa mapinduzi ya kijeshi Jenerali Abdel Fattah al-Burhan.

Sudan | Proteste gegen die Militärjunta in Khartum
Picha: AFP/Getty Images

Waandishi wa shirika la habari la AFP wamesema vikosi vya usalama vimeweka vizuizi vya barabarani kwenye daraja la mto Nile linalounganisha mji mkuu wa Khartoum na viunga vyake.

Kwa ujasiri mkubwa, waandamanaji hao wameapa kujitokeza kwa wingi barabarani kufuatia kipindi kifupi cha utulivu wakati wa sikukuu ya Eid-al-Adhaa iliyokamilika mapema wiki iliyopita.

Soma pia: Waliouawa mapigano ya Darfur wafikia 200

Waandamanaji wanapinga hatua ya Burhan kuchukua madaraka kwa nguvu mnamo mwezi Oktoba. Vilevile wameonyesha wasiwasi kutokana na kuzuka kwa mapigano makali katika jimbo la kusini mwa Sudan la Blue Nile, lililoko takriban kilomita 450 kusini mwa Khartoum.

Maandamano yamechochewa na jeshi kuvuruga mpango wa kurudisha utawala wa kiraia 

Mkuu wa jeshi la Sudan Jenerali Abdel-Fattah BurhanPicha: Marwan Ali/AP/picture alliance

Mapinduzi ya hivi karibuni ya Sudan yamevuruga kipindi cha mpito kuelekea utawala wa kiraia na kusababisha maandamano ya karibu kila wiki na ukandamizaji wa vikosi vya usalama ambao umesababisha vifo vya watu wapatao 114, kulingana na kamati kuu ya madaktari wa Sudan wanaounga mkono demokrasia.

Kamati hiyo ya madaktari imesema watu tisa waliuawa mnamo Juni 30, wakati maelfu ya watu walipoandamana na vifo hivyo vimechochea tena harakati za kuupinga utawala wa kijeshi.

Soma pia: Kiongozi wa wapiganaji ashitakiwa ICC kwa uhalifu Darfur

Mnamo Juni 4, katika hali ya kushangaza Burhan aliapa kutoa nafasi ya kurudisha utawala wa kiraia. Hata hivyo, kundi kuu la mwavuli wa mashirika ya kiraia walikataa pendekezo hilo na kulitaja kama "ujanja tu wa jeshi."

Waandamanaji wameendelea kumshinikiza mkuu wa jeshi kujiuzulu. Wanaushtumu utawala wa kijeshi uliopo madarakani sasa na viongozi wa waasi wa zamani ambao walitia saini mkataba wa amani wa mwaka 2020 kwa kuzidisha mivutano ya kikabila kwa manufaa yao kibinafsi.

 

Waandamanaji wakikabiliana na polisi katika mji mkuu KhartoumPicha: AFP

Katika jimbo la Blue Nile leo Jumapili, mashuhuda wamesema kuwa wanajeshi wametumwa katika mji wa Al-Roseires baada ya takriban watu 65 kuuawa na wengine zaidi ya 100 wamejeruhiwa katika ghasia za kikabila.

Kundi la wapiganaji katika jimbo la Blue Nile lilipambana na rais wa zamani Omar al-Bashir wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya mwaka 1983 hadi mwaka 2005, na wakachukua silaha tena mwaka 2011.

Bashir aliondolewa madarakani mwaka 2019. Mwaka uliofuata, utawala wa mpito ulifikia makubaliano ya amani na makundi ya waasi, yakiwemo makundi kutoka jimbo la Blue Nile na eneo lililoharibiwa kwa vita la Darfur Magharibi.

Ghasia za sasa katika jimbo la Blue Nile ni kati ya watu wa makabila ya Berti na Hausa.

Soma pia: Watu wanane wauawa na vikosi vya usalama nchini Sudan

Kwa mujibu wa taarifa za wizara ya afya, takriban watu 108 wamejeruhiwa na maduka 16 yametekezwa moto tangu ghasia hizo zilipozuka siku ya Jumatatu na ambazo zimechochewa na mzozo wa ardhi kati ya watu wa makabila ya Berti na Hausa.

"Tunahitaji wanajeshi zaidi kutuliza hali,” afisa wa serikali Adel Agar kutoka mji wa Al-Roseires aliliambia shirika la Habari la AFP jana Jumamosi. Afisa huyo amesema watu wengi walikuwa wanatafuta hifadhi katika vituo vya polisi na kwamba ghasia hizo zimesababisha vifo na majeruhi.

Waziri Mkuu Sudan asema hakuna atakaekwepa mkono wa sheria

01:03

This browser does not support the video element.

Agar hata hivyo hakutoa maelezo zaidi juu ya idadi ya wahanga japo ameongeza kuwa wapatanishi wanahitajika haraka ili kukomesha ghasia hizo. Wanajeshi wametumwa katika eneo hilo huku amri ya watu kutotoka nje usiku ikiwekewa na mamlaka kuanzia Jumamosi.

Gavana wa jimbo la Blue Nile Ahmed al-Omda amepiga marufuku mikusanyiko ya aina yoyote au kufanyika kwa maandamano kwa muda wa mwezi mmoja.

Ghasia hizo zilizuka baada ya watu wa kabila la Berti kukataa ombi la watu wa kabila la Hawsa la kuunda "mamlaka ya kiraia ya kusimamia upatikanaji wa ardhi,” mmoja wa mwanachama wa Hawsa ameliambia shirika la AFP kwa sharti la kutotajwa jina.

Hata hivyo mwanachama mkuu wa Bertis amesema kabila hilo lilikuwa linajibu kile walichokiita "ukiukwaji” wa ardhi zao uliofanywa na Hawsas.

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW