1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wa kigeni na wanadiplomasia kuondolewa nchini Sudan.

22 Aprili 2023

Kiongozi wa Sudan ambaye pia ni mkuu wa jeshi, Abdel Fattah al-Burhan, ameridhia kuhamishwa raia na wawakilishi wa kidiplomasia kutoka katika nchi hiyo iliyomo kwenye mzozo. Mapigano ya Sudan yameingia wiki ya pili.

Sudan | Kämpfe in Khartoum
Picha: AFP/Getty Images

Msemaji wa jeshi amesema katika taarifa yake siku ya Jumamosi kwamba Marekani, Uingereza, Ufaransa na China zitaanza shughuli za kuwahamisha raia wake kutoka kwenye mji mkuu wa Sudan, Khartoum katika muda usio mrefu kwa kutumia ndege za kijeshi.

Kiongozi na mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan.Picha: ASHRAF SHAZLY/AFP/Getty Images

Jeshi limesema mkuu wake, Jenerali Abdel Fattah Burhan, amezungumza na viongozi wa nchi kadhaa ambao wameomba raia na wanadiplomasia wao kuondolewa salama kutoka nchini Sudan.

Soma:Mapigano yazuka tena Sudan

Al-Burhan ameahidi kuwezesha na kudhamini zoezi la kuwahamisha watu na kuzipa nchi hizo msaada unaohitajika ili kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa.

Msemaji wa jeshi ameeleza kwamba wajumbe wa Saudi Arabia tayari umeondolewa kutoka kwenye mji wa mashariki wa Port Sudan. Amesema wajumbe wa Jordan pia wanatarajiwa kusafirishwa kwa ndege kutoka Port Sudan baadaye Jumamosi.

Kushoto kiongozi na Mkuu wa jeshi la Sudan Abdul Fattah Al-Burhan. Kulia: Kiongozi wa kikosi cha RSF Mohamed Hamdan Dagalo.Picha: Bandar Algaloud/Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance

Jordan imesema inafuatilia kwa karibu hali ya usalama ya nchini Sudan na kwamba inashirikiana na Saudi Arabia na nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu.

Soma:Mataifa zaidi kuwaondoa raia wao Sudan

Wizara ya ulinzi ya Marekani mapema wiki hii ilisema itawapeleka askari wa ziada na vifaa katika kituo cha wanamaji kilichopo Djibouti kwa ajili ya kujiandaa kwa zoezi la kuwaondoa wafanyakazi wa ubalozi wa Marekani. Wakati huo huo ikulu ya Marekani hadi siku ya Ijumaa ilisema serikali haikuwa bado na mpango wa kuratibu zoezi la kuwahamisha takriban raia 16,000 wa Marekani ambao wamekwama nchini Sudan.

Hata ingawa pande zinazopigana zilikubaliana kusitisha mapigano kwa siku tatu ili kutoa nafasi ya kuqdhimisha Sikukuu ya Eid al-Fitr, milipuko na milio ya risasi imeendelea kusikika kote katika jiji la Khartoum siku ya Jumamosi. Mara mbili makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa mapema wiki hii yalikiukwa ndani ya muda mfupi pia.

Wanajeshi wa Sudan wanaomtii mkuu wa jeshi Abdel-Fattah al-Burhan.Picha: Mahmoud Hjaj/Anadolu Agency/picture-alliance

Katibu wa muungano wa madaktari wa Sudan, unaofuatilia na kuratibu watu waliojeruhiwa Atiya Abdalla Atiya amesema watu wanapaswa kutambua kuwa vita vimekuwa vikiendelea tangu siku ya kwanza vilipoanza. Kulingana na ripoti ya Shirika la Afya Duniani, mapigano hayo yamesababisha vifo vya watu zaidi 400 kufikia sasa. WHO imesema watu wengine 3,551 wamejeruhiwa kwenye mgogoro huo wa Sudan.

Soma:Waliouawa Sudan wafikia 400, majeruhi wapindukia 3,500

Mkuu wa jeshi la Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan ameiambia televisheni ya Al Arabiya kwamba pande zinazopigana zinahitaji kukaa chini na kuzungumza kama Wasudan ili kutafuta njia sahihi ya kurejesha matumaini na hali ya maisha ya kawaida kwa watu wa nchi Sudan.

Vyanzo:AP/RTRE

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW