1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSudan

Jeshi la Sudan laukomboa uwanja wa ndege wa Khartoum

26 Machi 2025

Jeshi la Sudan limeuzingira na kuchukua udhibiti wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Khartoum siku ya Jumatano, wakati mapigano makali yakiendelea sehemu mbalimbali nchini humo kati ya jeshi na wanamgambo wa RSF.

Vita vya Sudan I Moshi ukifuka katika uwanja wa ndege wa Khartoum
Moshi ukifuka katika uwanja wa ndege wa Khartoum kufuatia mapigano kati ya jeshi na wanamgambo wa RSFPicha: AFP/Getty Images

Taarifa ya kukombolewa kwa uwanja wa ndege kutoka mikononi mwa wanamgambo wa RSF imetolewa na msemaji wa jeshi la Sudan, Nabil Abdallah aliyethibitisha kwamba vikosi vyao sasa vinaulinda kikamilifu uwanja huo wa ndege unaopatikana katikati mwa jiji.

Kulingana na taarifa ya jeshi, vikosi vyao zinaendelea na mapigano kwenye eneo la kusini mwa Khartoum na kwamba vimelizingira eneo la kimkakati la Jebel Awliya, na kusisitiza kuwa wanamgambo wa RSF waliosalia sasa wameanza kukimbia kwa kuvuka mto katika jimbo la White Nile kwa kutumia daraja la Jebel Awliya ambalo ndio njia pekee ya kuondoka eneo hilo.

Mafanikio haya yanajiri siku moja baada ya jeshi la Sudan  kushutumiwa kwa shambulio baya zaidi la anga katika soko huko magharibi mwa Darfur na kuwaua takriban watu 270. Milio ya risasi hata hivyo imeendelea kusikika mjini Khartoum.

Jeshi la Sudan lajiimarisha na kuikabili zaidi RSF

Baada ya kuimarisha vikosi na silaha zake, jeshi la Sudan linaonekana kukaribia kuudhibiti kabisa mji mkuu Khartoum, ambao serikali yake ililazimika kuukimbia mwanzoni mwa vita na kuelekea katika mji wa Bahari ya Shamu wa Port Sudan.

Jeshi hilo lilianzisha wiki iliyopita operesheni kabambe ya kupambana na wanamgambo wa RSF  kwa lengo la kuwafurusha katika mji mkuu Khartoum walipokuwa wameweka ngome yao. Ijumaa iliyopita, jeshi liliikomboa Ikulu ya Rais na kuchukua udhibiti wa majengo ya taasisi kadhaa za serikali.

Mkuu wa jeshi la Sudan Jenerali Abdel Fattah al-BurhanPicha: Sudanese Army/AFP

Video iliyopeperushwa kwenye mitandao ya kijamii na ambayo haikuweza kuthibitishwa na vyanzo huru, imewaonyesha wakazi wa Khartoum wakisherehekea kufuatia pigo hilo kwa wanamgambo wa RSF. Mkazi wa Khartoum Osama Abdel Qader ameeleza kuwa wanamgambo wameonekana wakiondoka katika baadhi ya nyumba walizokuwa wakiishi na kuondoka na baadhi ya vitu.

Soma pia: Takriban watu 61 wauawa katika shambulizi la anga, Darfur

Tangu kuanza kwa vita, RSF imekuwa ikilaumiwa kwa kukalia kwa mabavu makazi ya raia, kuwapora mali zao, kuhusika na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na kadhalika. Hata hivyo jeshi na RSF wote wamekuwa wakishutumiwa kwa kuwalenga raia na kushambulia kiholela maeneo ya makazi.

Marekani iliwawekea vikwazo mahasimu wawili katika mzozo huo ambao ni mkuu wa majeshi Abdel Fattah al-Burhan na makamu wake wa zamani, kamanda wa RSF Mohamed Hamdan Daglo. Vita vya Sudan vilivyoanza Aprili mwaka 2023, vimesababisha vifo vya maelfu ya watu, huku mamilioni ya wengine wakilazimika kuyahama makazi yao.

(Vyanzo: AP, Reuters)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW