1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Syria lajiandaa kuisafisha Aleppo

Sylvia Mwehozi
21 Desemba 2016

Jeshi la Syria limewataka waasi na raia waliosalia katika eneo la mwisho la upinzani mjini Aleppo kuondoka wakati likijiandaa kuuchukua kikamilifu mji huo.

Syrien  Aleppo Evakuierung
Picha: Reuters/Sana

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa mataifa matatu ya Urusi, Iran na Uturuki wamekubaliana juu ya umuhimu wa kutanua usitishwaji wa mapigano. 

Serikali na pande zote katika mzozo wa Syria zimekubaliana kuwaruhusu waangalizi 20 kupelekwa nchini humo ili kufuatilia zoezi hilo, kwa mujibu wa msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric.

Katika mkutano wa hapo jana baina ya mataifa matatu ya Urusi, Iran na Uturuki uliokuwa na lengo la kufufua mchakato wa amani, mawaziri wa mambo ya kigeni wamekubaliana juu ya umuhimu wa kupanua usitishwaji mapigano, upatikanaji wa misaada ya kiutu pamoja na kuwahamishia raia katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali.

Mawaziri wa kigeni wa Urusi, Iran na Uturuki mjini MoscowPicha: picture-alliance/AP Photo/P. Golovkin

Mevlut Cavusoglu waziri wa mambo ya nje wa Uturuki ameelezea baadhi ya yaliyogusiwa akisema kuwa "tunaamini kuwa usitishaji mapigano haupaswi kuyalinda makundi ya kigaidi kama Al Nusra na IS. Lakini yapo makundi mengine ambayo yanafungamana na serikali kwa mfano Hezbollah na ni muhimu kuacha kuyaunga mkono. Katika kesi kama hii itawezekana kusitisha mapigano, lakini hatupaswi kunyoosha kidole dhidi ya kundi moja au upande mmoja, pande zote zisitishe mapigano" alisema waziri huyo.

Mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov ambaye alikuwa ni mwenyeji wa mazungumzo hayo hakubishana kiuwazi na kauli ya waziri wa Uturuki lakini akaweka bayana msimamo wa nchi yake kwamba makundi yaliyoingia nchini humo yapo kwasababu yamealikwa na serikali ya rais Bashar al- Assad na hivyo jukumu lao ni kupambana magaidi. 

Alipulizwa kuhusu upinzani wa Uturuki kulihusu kundi la Hezbollah, Waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema nchi hiyo inaheshimu msimamo huo lakini hata hivyo nchi nyingine hazikubaliani na maoni hayo.

Huko mashariki mwa Aleppo, askari wametoa mwito kwa wapiganaji waliosalia na raia kuondoka katika wilaya ya upinzani, wakati jeshi likijiandaa kuusafisha. Navyo vikosi vya jeshi la Uturuki vimedai kulitwaa eneo lililokuwa mikononi mwa kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS la Al-Bab ambalo ni njia kuu inayounganisha mji wa Aleppo kufuatia mashambulizi makali ya ardhini na angani.

Mwanaume katika baiskeli ya walemavu akiondoka mjini AleppoPicha: Reuters/A.Ismail

Kiasi ya watu 25000 wameripotiwa kuondoka tangu lilipoanza zoezi la kuwahamisha raia wiki iliyopita, kwa mujibu wa kamati ya kimataifa ya msalaba mwekundu, ambao wanafuatilia operesheni hiyo.

Mbali na mabasi 10 yaliyoondoka jana Jumanne, hakuna mabasi mengine yaliyoshuhudiwa kuondoka na raia, limesema shirika linaloangalia haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake makuu Uingereza.

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa siku ya jumatatu zilipitisha azimio lililoandaliwa na Ufaransa ili kufuatilia zoezi la kuwaondoa rais Aleppo.

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa Syria Staffan de Mistura amesema anayo matumaini ya kuitisha mazungumzo mapya ya amani mjini Geneva hapo Februari mwakani.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP/REUTERS

Mhariri: Daniel Gakuba