Jeshi la Syria lapambana kukomboa vyanzo vya maji Damascus
27 Desemba 2016Majeshi ya serikali ya Syria yalishambulia kwa mabomu miji kadhaa katika bonde la ufa la Wadi Barada lililo umbali wa kilomita 18 kutoka upande wa kaskazini Magharibi mwa mji mkuu wa Damascus. Operesheni hiyo kubwa ilianzishwa tangu siku ya ijumaa katika eneo hilo. Maeneo yanayolizunguka eneo hilo yako mikononi mwa majeshi ya serikali yakishirikiana na wapiganaji wa kundi la Hezbollah.
Waasi wamesema kuwa wanajeshi wa Syria wameongeza nguvu baada ya ushindi wa kuukomboa mji wa Aleppo hivyo basi waasi hao wanakabiliwa na hali ngumu ambapo wanapaswa kuchagua kuondoka kwa hiari au kukabiliwa na vita vikali. Kamanda wa waasi hao Said Abu al Baraa amesema hawatakubali kamwe kuiachia ardhi yao ya Ahrar al Sham.
Kufuatia mfululizo wa mashambulizi ya kijeshi, serikali ya Syria ikisaidiwa na ndege za Urusi mshirika wake mkuu imekuwa ikiwakabili vikali wapinzani wenye silaha katika mji mkuu. Chanzo cha maji cha Wadi Barada kipo Damascus kwenye njia ya kuelekea katika mpaka wa Lebanon. Wapiganaji wa kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran wanatumia njia hiyo kwa ajili ya kusafirishia mahitaji. Kundi hilo linashiriki katika vita vya Syria kwa upande wa rais Bashar al Assad.
Jeshi la Syria limewalaumu waasi kwa uchafuzi wa vyanzo vya maji kutokana na kumwaga mafuta ya diseli katika vyanzo hivyo hatua ambayo imeilazimu idara ya maji kukatiza huduma hiyo kuelekea katika mji mkuu. Kwa upande wao waasi hao wamekanusha shutuma dhidi yao. Waasi wamekuwa wakiiruhusu idara ya maji ya serikali kusimamia kituo hicho cha maji tangu walipolidhibiti eneo hilo mnamo mwaka 2012. Waasi hao ni mchanganyiko wa wapiganaji kutoka kwenye makundi ya dola la kiislamu IS na Jeshi huru la Syria, Free Syrian Army. Mara kwa mara waasi hao wamekuwa wakikatiza huduma ya maji hatua ambayo wamekuwa wakiitumia kama turufu ya kulizuia jeshi la serikali lisianzishe operesheni ya kuukomboa mji huo.
Wakati huo huo vyombo vya habari nchini Ujerumani vimeripoti kwamba serikali inapanga kutoa msaada wa Euro milioni 15. Fedha hizo zitatumika kugharamia kazi za madaktari, wauguzi na watalaamu wa Syria wapatao 1000 kwa muda wa miezi 30.Waziri wa Ujerumani wa misaada ya maendeleo Gerd Müller ameliambia gazeti la "Bild" kwamba baada ya jumuiya ya kimataifa kushindwa kuzuia mauaji na mashambulio sasa inapaswa kutekeleza mpango kabambe wa misaada ya kibinadamu kwa ajili ya watu wa Aleppo. Umoja wa Mataifa umesema kwa sasa watu zaidi ya milioni 13.5 nchini Syria wanahitaji misaada ya kibinadamu. Kwa upande wake Saudi Arabia imeanzisha kampeni ya kuwachangia Wasyria walioathirika kwa vita vya miaka mitano vya wenyewe kwa wenyewe. Zaidi ya Wasyria milioni 11 wamelazimika kuyahama makaazi yao kutokana na vita vilivyoanza mwaka 2011. Watu zaidi ya laki 3 wameuwawa.
Mwandishi: Zainab Aziz/RTRE
Mhariri: Josephat Charo