Jeshi la Syria, washirika waanza kuushambulia mji wa Daraa
27 Juni 2018Vikosi vya serikali vimeelekeza nguvu katika kulirejesha chini ya udhibiti wake eneo hilo la kimkakati linalopakana na Jordan na upande wa milima ya Golan unaodhibitiwa na Israel.
Mapambano hayo dhidi ya waasi ndiyo ya karibuni zaidi katika kampeni inayoungwa mkono na Urusi kurejesha maeneo ambayo serikali iliyapoteza tangu kuanza kwa vita vya Syria mwaka 2011.
Umoja wa Mataifa unakaridia karibu Wasyria 45,000 wameyapa kisogo makaazi yao tangu vikosi vya serikali na washirika wake walipoanzisha mashamhulizi wiki moja iliopita.
Msemaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu masuala ya kibinadamu Jens Laerke, alisema wale wanaokimbia mapigano mkoani Daraa walikuwa wanakaribia mpaka uliofungwa wa Jordan, huku wakiwa hawana njia dhahiri ya kutorokea.
Akizungumza mjini Geneva Uswisi hapo jana, Laerke alisema shirika lake lina wasiwasi hasa kuhusu usalama wa watu takribani 750,000 waliozingirwa katika mapigano hayo.
"Tunazo ripoti za watu wasiopungua elfu 45 ambao tayari wamekuwa wakimbizi wa ndani, kiasi ya watu kati elfu 45 na 50 tayari," alisema Laerke katika mkutano na waandishi habari.
Baraza la wakimbizi Norway laisihi Jordan
Msemaji wa serikali ya Jordan alisema mapema wiki hii kuwa nchi hiyo ya Kifalme haitachukuwa wakimbizi zaidi kutoka Syria. Jordan tayari inawahifadhi karibu wakimbizi 660,000 kutoka Syria na inakisiwa kwamba idadi yao ni mara mbili zaidi.
Baraza la Wakimbizi la Norway hata hivyo limeisihi nchi hiyo kuwafungulia mipaka wakimbizi hao ambao limesema hawana mahala pengine pa kwenda. Shirika hilo la kimataifa la misaada limesema Jordan haiwezi kutarajiwa kubeba mzingo huo pekee yake.
Linasema jumuiya ya kimataifa laazima itoe msaada wa maana, na kwamba mashirika ya misaada yako tayari kusaidia kuwaweka wakimbizi wapya wanaowasili katika kambi ya Azraq, ambayo limesema inaouwezo wa kuwahifadhi watu elfu 80 zaidi.
Mji wa Daraa ambao unabeba jina sawa na mkoa na ndiyo ulikuwa chimbuko la uasi ulioanza 2011 dhidi ya rais Bashar al Assad, umegawanyika kati ya waasi wanaodhibiti sehemu ya kusini, wakati upande wa kaskazini ukiwa mikononi mwa vikosi tiifu kwa utawala.
Shirika la uangalizi wa haki za binadamu la Syria lenye makao yake jijini London, Uingereza, limesema tangu kuanza kwa operesheni hiyo kubwa mashariki mwa Daraa Jumanne wiki iliopita, raia 32, waasi 29 na wanajeshi 24 wa serikali wameuawa katika mashambulizi ya angani na mapigano.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae,afpe,aptn
Mhariri: Saumu Yusuf