Jeshi la Ufaransa CAR kuongezewa muda
6 Februari 2014Waziri Jean Yves Le Drian ametangaza azma ya kurefusha muda wa wanajeshi wa Ufaransa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, kupitia kituo kimoja cha redio cha Ufaransa. Le Drian amesema kwa sasa vikosi vya vinao ujumbe utakaodumu kwa miezi sita, kipindi ambacho amesema kitaorefushwa. Waziri huyo amesema hatimaye ujumbe wa Umoja wa Mataifa utahitajika katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambao utahitaji walinda amani.
Aidha waziri huyo ameonya juu ya uwezekano wa nchi hiyo, Jamhuri ya Afrika ya Kati, kusambaratishwa na mizozo, ikitiliwa maanani kuwa inapakana na maeneo ya Maziwa makuu na ukanda wa Sahel, ambayo yana historia ya majanga.
Miezi miwili iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliidhinishwa kupelekwa kwa wanajeshi wa Ufaransa na vikosi vya kiafrika katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, kuingilia kati katika mgogoro wenye umwagaji wa damu ambao ulikuwa ukishamiri. Ufaransa inao wanajeshi 1600 katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambao wanasaidiana na wengine takribani 5000 kutoka mataifa ya Kiafrika kulinda amani nchini humo.
Le Drian amesema wanajeshi hao wameweza kuepusha shari kamili katika nchi hiyo yenye wakazi milioni nne, ambao robo yao wameyakimbia makazi yao, kukimbia ghasia ambazo zimeendelea kwa karibu mwaka mzima, mauaji ya mara kwa mara, na hali mbaya ya kibinadamu.
Wanajeshi wamuuwa raia hadharani
Haya ameyasema Jean Yves Le Drian siku moja baada ya Marekani kuitolea wito Jamhuri ya Afrika ya Kati kusimamisha ghasia na ulipaji kisasi, baada ya wanajeshi wa serikali kumuuwa mbele ya kadamnasi mtu aliyeshukiwa kuwa mpiganaji wa waasi, hapo jana.
Kisa hicho cha kuogofya ambacho kilifanywa mbele ya wapigapicha, kilitokea muda mfupi baada ya tangazo la rais wa mpito wa nchi hiyo Bi Catherine Samba Panza kuelezea fahari aliyonayo kutokana na juhudi za jeshi la serikali kuchangia katika kurejesha usalama nchini mwao.
Waandishi wa habari walishuhudia wanajeshi waliovaa sare za jeshi la taifa, wakimshambulia kijana aliyevaa nguo za kiraia. Wanajeshi hao walipiga mateke kichwani, walimcoma visu na kumponda kijana huyo hadi kufa. Afisa mmoja alisikika akiongea kwa sauti kubwa, na kusema kijana huyo alikuwa kutoka kundi la waasi wa Seleka. Umati wa watu ulijiunga na wanajeshi katika kumshambulia.
Maiti ya kijana huyo iliburirwa mitaani, huku wanajeshi wa ujumbe wa Umoja wa Afrika, MISCA, wakiangalia tu.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani Jennifer Psaki alisema nchi hiyo inatiwa wasiwasi na kuendelea kwa makabiliano baina ya makundi ya wakristo na ya waislamu. Psaki aliushauri uongozi mpya wa mpito wa nchi hiyo, kutumia vyema uungwaji mkono wa kimataifa kuumaliza mgogoro na kuandaa mustakabali mwema kwa nchi.
Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/RTRE
Mhariri: Mohammed Khelef