Jeshi la Ukraine lauhama uwanja wa Donetsk
22 Januari 2015Uamuzi huo wa serikali ya Ukraine kuwaondoa wanajeshi wake katika uwanja mkuu wa ndege katika mji wa Donetsk umefikiwa baada ya miezi kadhaa ya mapigano dhidi ya waasi kuwania udhibiti wa uwanja huo. Hata hivyo jeshi la nchi hiyo limesisitiza kuwa sehemu ya uwanja huo bado iko chini ya ulinzi wake. Jana, mwandishi mmoja wa kituo cha televisheni cha Ukraine aliutembelea uwanja huo na kuonyesha picha za miili ya wanajeshi wa serikali waliouawa.
Mapigano katika uwanja huo yaliongezeka sana mwishoni mwa juma lililopita, na kuvuruga utulivu ambao ulikuwa ukishuhudiwa katika eneo hilo baada ya makubaliano ya kusitisha uhasama yaliyosainiwa mwezi Desemba baina ya jeshi la serikali na waasi wa mashariki wanaotaka kujitenga. Umoja wa Mataifa unakadiria kwamba vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoanza Aprili mwaka jana, vimeuwa watu zaidi ya 4,700.
Diplomasia sambamba na vita
Hali hiyo ya kivita imeendelea licha ya juhudi za kidiplomasia ambazo ziliendelea katika mji mkuu wa Ujerumani Berlin hadi usiku wa kuamkia leo, zikiwashirikisha mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Ukraine, Urusi, Ufaransa na mwenyeji Ujerumani. Mazungumzo ya wanadiplomasia hao yaliazimia kufufua majadiliano yaliyovunjika wiki iliyopita, ambayo yalihusu utekelezwaji wa makubaliano ya kusitisha vita yaliyofikiwa mwezi Septemba 2014, katika mji mkuu wa Belarus, Minsk.
Katika tangazo lake kwa vyombo vya habari baada ya mazungumzo hayo, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier alisema kuna dalili za mafanikio.
''Hatimaye leo tumepata muafaka juu ya mpaka ambao kwa mujibu wa makubaliano ya mjini Minsk, kulingana na mambo yalivyo kwa wakati huu, ni eneo ambalo silaha nzito zinapaswa kuondolewa. Tumekubaliana juu ya mpaka huo pamoja na mambo mengine.'' Amesema Steinmeier.
Hali kadhalika, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ukraine Pavlo Klimkin alitoa kauli ya matumaini, akisema mapatano yaliyofikiwa ikiwa ni pamoja na mazungumzo zaidi, yanaweza kuwa na matokeo mazuri. ''Ni matumaini yangu kuwa pande zote zinazohusika zitashirikiana katika juhudi hizo'', amesema waziri huyo.
Poroshenko atoa cheche
Lugha hiyo ya maridhiano na matumaini ilikuwa tofauti na maneno yaliyotamkwa na rais wa Ukraine Petro Poroshenko katika kongamano la kiuchumi linaloendelea mjini Davos, Uswisi. Rais huyo alisema vita mashariki mwa nchi yake vitasimama tu, ikiwa Urusi itaacha kuwasaidia waasi kwa silaha na wapiganaji. Alisema, ''Msimamo wetu ni rahisi, hakuna cha kuzungumza. Ikiwa maoni yako ni tofauti na msimamo wetu, maana yake hutaki amani, unataka vita''.
Taarifa za hivi karibuni kutoka mashariki mwa Ukraine zinaeleza kuwa watu wasiopungua 13 wameuawa baada ya kushambuliwa kwa basi walilokuwa wakisafiria. Ukraine imewatuhumu waasi kufanya mashambulizi hayo.
Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/DPAE/APE
Mhariri:Yusuf Saumu