1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Uturuki laingia Syria dhidi ya IS

24 Agosti 2016

Uturuki imepeleka vifaru katika mji wa Jarablus Kaskazini mwa Syria katika operesheni dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu. Hayo yanajiri wakati Makamu wa Rais wa Marekani Joe Biden akianza ziara nchini Uturuki.

Vifaru vya Uturuki vikiwa njia kuelekea Syria
Vifaru vya Uturuki vikiwa njia kuelekea SyriaPicha: picture-alliance/AA/E. Ozdemir

Ripoti ambazo zimezinukuu duru za kijeshi, zimesema operesheni hiyo ya jeshi la Uturuki iliyopachikwa jina la ''Ngao ya Euphrates'' imeanza leo kabla ya mapambazuko. Serikali ya Uturuki imesema operesheni hiyo inasaidiwa na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS. Makundi kadhaa ya waasi wa Syria hali kadhalika yamesema yameingiza wapiganaji wao katika mji wa Jarablus, kupambana na wanamgambo wa IS.

Akizungumza muda mfupi uliopita mjini Ankara, rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amethibitisha kuanza kwa operesheni hiyo, na kuongeza kuwa nchi yake inaazimia kuhakikisha wasyria wanakuwa na udhibiti wa nchi yao wenyewe. Erdogan amesema ikiwa lazima, Uturuki itajitwisha jukumu la kuhakikisha kuwa azma hiyo inafikiwa.

Operesheni yashirikisha muungano unaoongozwa na Marekani

Awali ofisi ya waziri mkuu wa Uturuki imesema operesheni ''Ngao ya Euphrates'' ambayo ndio kubwa zaidi kuwahi kufanywa na Uturuki nchini Syria inashirikisha vikosi vya anga na vya nchi kavu, na kwamba shabaha yake ni kuukomboa mji wa Jarablus kutoka mikononi mwa makundi ya wanajihadi. Mji huo uko kwenye mpaka baina ya Uturuki na Syria.

Hii ndio operesheni kubwa zaidi ya Uturuki ndani ya SyriaPicha: Getty Images/AFP/B. Kilic

Ndege za jeshi la Uturuki chapa F-16 na nyingine za muungano unaoongozwa na Marekani zimepiga maeneo kadhaa ndani ya Syria, na mpiga picha wa shirika la habari la AFP ameshuhudia msafara wa vifaru vya Uturuki ukivuka mpaka kuingia Syria.

Wakati huo huo makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden amewasili leo nchini Uturuki, ikiwa ziara ya kwanza ya kiongozi wa ngazi ya juu wa wa nchi ya Magharibi kuizuru Uturuki, tangu kushindwa kwa jaribio la mapinduzi dhidi ya utawala wa rais Erdogan, hapo Julai 15.

Biden awasili kupunguza mvutano

Biden atataka kupunguza mvutano kati ya nchi yake na Uturuki ambayo ni mwanachama wa Jumuiya ya Kujihami, NATO, hususan kuhusu kuwepo nchini Marekani kwa Ulamaa wa Kituruki Fethullah Gulen, ambaye utawala wa Rais Erdogan unamtuhumu kuwa kinara wa jaribio la mapinduzi lililoshindwa.

Makamu wa Rais wa Marekani Joe BidenPicha: picture-alliance/AP Photo/N. Ut

Uturuki imekuwa ikiishinikiza Marekani kumrejesha nyumbani Gulen ambaye anakanusha vikali kuhusika kwa njia yoyote ile na jaribio hilo.

Tofauti nyingine kubwa kati ya Uturuki na Marekani ni kuhusu kundi la wanamgambo wa Kikurdi la YPG, ambalo linachukuliwa na Uturuki kama kundi la kigaidi, wakati Marekani ikilichukulia kama mshirika muhimu katika vita vya Syria.

Katika operesheni yake ya kijeshi nchini Syria, Uturuki inakusudia kuonyesha kuwa haina mzaha katika kulishughulikia kundi la IS, ambalo limeshutumiwa kufanya mashambulizi kadhaa ya kigaidi nchini Uturuki, likiwemo la Jumapili iliyopita lililouwa watu 54 waliokuwa kwenye sherehe za arusi katika mji mwingine wa mpakani wa Gaziantep.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/dpae

Mhariri: Mohammed Khelef