1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi laahidi kurejesha usalama Burkina Faso

28 Januari 2022

Kiongozi wa utawala wa kijeshi nchini Burkina Faso ameahidi kurejesha usalama, utulivu na umoja katika nchi hiyo iliyomo katika mgogoro. Hata hivyo ameonya kuwa usaliti hautavumiliwa na utawala wake mpya.

Burkina Faso | Neue Militärjunta
Picha: Radio Télévision du Burkina/AFP

Kiongozi huyo, luteni kanali Paul Henri Sandaogo Damiba amelihutubia taifa kwa mara ya kwanza tangu kutwaa mamlaka mapema wiki hii baada ya kumwondoa madarakani rais Roch Kabore aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia. Kiongozi huyo wa kijeshi pia ameitaka jumuiya ya kimatifa iiunge mkono nchi yake ili iweze kuanza tena juhudi za kuelekea kwenye maendeleo.

Akizungumza kutoka ikulu, kanali Damiba amesema, Burkina Faso inakabiliwa na mgogoro usiokuwa na kifani na hivyo jukumu la kipaumbele kwa utawala wake wa kijeshi ni kurejesha usalama, kuimarisha ari ya wanajeshi na kusikiliza maoni ya wananchi.

Rais wa Burkina Faso aliyeondolewa madarakani na jeshi Roch Marc Christian KaboréPicha: PREFASO

Amesema tayari ameanza mashauriano na baadhi ya makundi kwenye taifa hilo, ikiwa ni pamoja na watu waliokuwemo katika utawala ulioondolewa madarakani, ili kubainisha misimamo mikuu ambayo hatimaye itawezesha kupatikana maamuzi ya maridhiano na jumuishi kwa ajili ya kuijenga Burkina Faso upya na kurejesha amani ya kudumu nchini humo.

Soma Zaidi:Jeshi Burkina Faso lakemewa licha ya uungwaji mkono

Tangu jeshi lilipotwaa madaraka, limetumia siku hizo chache kujaribu kupata uungwaji mkono kutoka kwa viongozi wa kidini, wa kijamii, kwa vikosi vya usalama pamoja na vyama vya wafanyakazi. Moussa Diallo, Katibu Mkuu wa Umoja wa wafanyakazi amesema utawala huo wa kijeshi ulikutana na wawakilishi wa chama cha wafanyakazi nchini humo katika ikulu jana Alhamis na kueleza sababu zake za kufanya mapinduzi na kwamba jeshi lina nia ya kurekebisha dosari za utawala uliopita.

Jumuiya ya kimataifa imelaani mapinduzi hayo, licha ya kwamba wananchi wanawaunga mkono wanajeshi. Wizara ya mambo ya nje ya Marekani katika taarifa yake imeonyesha wasiwasi mkubwa kuhusu kung'olewa madarakani serikali na kuvurugwa katiba nchini Burkina Faso na pia kuwekwa kizuizini kwa viongozi wa serikali.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: John Minchillo/POOL/AP/picture alliance

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema Katibu Mkuu Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa viongozi wa kijeshi kuweka chini silaha na kwamba amesisitiza juu ya kuzingatiwa ahadi kamili ya Umoja wa Mataifa ya kufwata utaratibu wa katiba nchini Burkina Faso na kutoa msaada kwa wananchi katika juhudi zao za kutafuta suluhisho kwa  changamoto nyingi zinazoikabili nchi hiyo.

Soma Zaidi:Burkina Faso kukabiliwa na hali tete zaidi? 

Jumuiya ya kiuchumi ya Afrika Magharibi, ECOWAS, pia imelaani mapinduzi hayo na nchi wanachama wa jumuiya hiyo zinatarjiwa kufanya mkutano hii leo Ijumaa kujadili uasi wa nchini Burkina Faso.

Vyanzo:AP/RTRE/AFP