1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi lamvua madaraka Bashir

Sekione Kitojo
11 Aprili 2019

Rais wa Sudan Omar al-Bashir ameondolewa madarakani na jeshi hali iliyotokana na maandamano yaliyofanyika kwa miezi ya kuipinga serikali, waandamanaji wakidai ajiuzulu baada ya miongo mitatu ya utawala wake wa kimabavu.

Omar al-Bashir
Picha: picture-alliance/AP Photo/H. Ammar

"Kamati ya usalama imeamua, ikiwa  ni  pamoja  na  majeshi  ya ulinzi  na  wadau wengine, kutekeleza  kile  kiongozi wa serikali hakuweza  kufanya, na kuchukua  jukumu  kamili  la  kubadilisha serikali yote katika  muda  wa  mpito  wa  miaka  miwili  ambapo majeshi  ya  ulinzi kimsingi yatachukua  uongozi  wa nchi  na  kuzuwia umwagikaji wa damu  pamoja  na  uwakilishi wa  kiasi  kutoka kamati ya usalama."

Waandamanaji wakishangiria kuondolewa madarakani kwa rais Omar al-Bashir mjini KhartoumPicha: Reuters

Waziri wa ulinzi  wa  Sudan alitangaza  leo kwamba  jeshi limempindua  na  kumkamata  rais Omar al-Bashir na  kuchukua madaraka  ya  nchi  kwa  miaka  miwili  ijayo  kufuatia  karibu  miezi minne ya  maandamno dhidi  ya  utawala  wake. Awad Mohammed Ibn Ouf  alionekana  katika  televisheni  ya  taifa  akivalia  sare  za jeshi , kufuatia  tangazo  la  hapo  kabla , kuhusu " taarifa muhimu, kutoka  katika  jeshi  leo  Alhamis.

Ibn Ouf  amesema  baada  ya  miaka  miwili , uchaguzi  huru  na  wa haki  utafanyika.

Wanajeshi wakisalimiana na wananchi waliojitokeza kuandamana kupinga tawala wa rais BashirPicha: picture-alliance

Amesema  amri  ya  hali  ya  hatari  imewekwa  kote  nchini  kwa muda  wa  miezi  mitatu na  kwamba  jeshi  pia  limesitisha  katiba  ya nchi  hiyo, kufunga  mipaka  na  anga  ya  nchi  hiyo.

"Pia  natangaza  kuundwa  kwa  baraza  la  mpito  la  jeshi  ambalo litatawala kwa  miaka  miwili, kusitisha katiba ya mpito  ya  Sudan iliyopitishwa mwaka  2005. Natangaza  hali  ya  hatari kwa  miezi mitatu na amri ya kutotembea usiku kwa mwezi  mmoja, kuanzia  saa 4 usiku  hadi  saa 10  alfajiri. Nafunga  anga ya Sudan kwa  masaa 24 pamoja  na  bandari  zote  za  kuingilia  Sudan  hadi itakapotangazwa  tena. Pia navunja  taasisi  ya  rais na  bunge."

Ummati wa watu ukiwa pamoja na wanajeshi wa Sudan baada ya jeshi kutangaza kumvua madaraka rais Omar al-BashirPicha: Getty Images/AFP

Idara za usalama pia zimetangaza  kuwaacha  huru  wafungwa  wote wa  kisiasa. Pamoja  na  hayo  waandamanaji  wamekataa tangazo hilo  la  jeshi  na  kusema  maandamano  yataendelea  kwa  kuwa hicho  ndio  walikuwa  wakipambana  nacho. Maelfu ya watu waliingia  katika  mitaa  ya  mji  mkuu  Khartoum  leo  kuandamana dhidi  ya  tangazo  hilo  la  jeshi  kwamba  rais Omar al-Bashir ameondolewa  na  nafasi  yake  itachukuliwa  na  baraza  la  mpito litakaloongozwa  na  jeshi.

Hali ya waandamanaji  ambao  hapo  kabla  walikuwa  wakishangilia iligeuka  kuwa  hasira , wengi  wakiimba , anguko  jingine, wakichukua  nyimbo  walizokuwa  wakiimba  hapo  kabla  za kumpinga Bashir.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW