1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi limeukomboa mji wa Shewa Robit, Ethiopia

1 Desemba 2021

Vikosi vinavyounga mkono serikali ya Ethiopia vimetangaza kwamba vimeukomboa mji wa Shewa Robit takriban kilomita 220 kutoka mji mkuu Addis Ababa.

Abiy Ahmed Äthiopien
Picha: picture-alliance/AP Photo

Baada ya waasi wa Tigray wiki iliyopita kudai kuudhibiti mji huo katika juhudi zao ya kuukaribia mji mkuu. Soma Abiy asema yuko tayari kuongoza mapambano dhidi ya TPLF

Msemaji wa serikali Legesse Tulu amesema Shewa Robit ni miongoni mwa miji midogo mingi iliyokombolewa na vikosi vilivyo chini ya amri ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed, ambaye wiki iliyopita alitangaza kuwa ataelekea kwenye uwanja wa vita huku mapigano yakiripotiwa kupamba moto, yakifuata mielekeo mitatu.

Mgogoro huo ulichukua mkondo mpya mwezi mmoja uliopita, wakati TPLF ilipodai kuteka miji ya kimkakati ya Dessie na Kombolcha, iliyoko kwenye barabara kuu kuelekea mji mkuu Addis Ababa.

soma Ni marufuku kutoa taarifa za harakati za kijeshi Ethiopia

Legesse ameongeza kuwa katika muda mfupi serikali ilichukua tena udhibiti wa mji wa Dessie na Lalibela, eneo la turathi la shirika la kimataifa UNESCO ambalo lilichukuliwa na waasi mnamo mwezi Agosti.

Onyo kutoka kwa Abiy

Picha: Amanuel Sileshi/AFP

Katika siku za hivi karibuni, vyombo vya habari vya serikali vimechapisha picha za waziri mkuu Abiy akiwa amevalia sare za jeshi katika eneo linaloonekana kuwa kaskazini mashariki mwa jimbo la Afar.

Abiy ni luteni kanali wa zamani katika jeshi la Ethiopia. Abiy amesema: "Vijana wa Kitigraya wanaanguka kama majani, watambue kuwa wameshindwa na wajisalimishe kuanzia leo kwa Jeshi la Ulinzi, vikosi maalum na wananchi kwa kuelewa kuwa wanashiriki kitu ambacho hakina maono au mpango wazi na ni safari isio na muelekeo na iliyochanganyikiwa, na haina hatima na haiwezi kupata ushindi."

Soma Waziri Mkuu Ahmed awaongoza wanajeshi vitani

Hofu ya waasi kusogea karibu na Addis Ababa imezifanya Marekani, Ufaransa, Uingereza na nchi nyingine kadhaa kuwataka raia wao kuondoka Ethiopia haraka iwezekanavyo, ingawa serikali ya Abiy inasema mafanikio ya TPLF yamedhibitiwa na mji uko salama.

Picha: Ethiopian News Agency/AP Photo/picture alliance

Vita hivyo vimesababisha hofu kubwa miongoni mwa mataifa ya Magharibi, hasa Marekani, ambayo wakati fulani ilimwona Abiy kama mwanamageuzi na mshirika mkuu.

Ingawa Washington imekuwa ikikosoa waziwazi jinsi Abiy anavyoshughulikia mgogoro huo, China na Urusi zimekuwa zikijizuia kuweka bayana misimamo yao.

Wizara ya mambo ya nje ya Ethiopia ilichapisha picha za mkutano na waandishi wa habari na mwanadiplomasia mkuu wa China Wang Yi wakati wa ziara yake nchini humo, na kumnukuu akisema "China inapinga uingiliwaji kwa aina yoyote katika masuala ya ndani ya Ethiopia."

soma UN yatoa fedha za msaada wa dharura Ethiopia

Kulingana na makadirio ya Umoja wa Mataifa mapigano hayo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu, zaidi ya milioni mbili kuyahama makazi yao na kusababisha maelfu kutumbukia katika  hali inayofanana na baa la njaa.

 

/afpe, rtre

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW