1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNiger

Jeshi na wananchi waunga mkono mapinduzi ya Niger

Sylvia Mwehozi
27 Julai 2023

Jeshi la Niger limetangaza kuwaunga mkono viongozi wa mapinduzi likisema kwamba kipaumbele chake ni kuepusha taifa hilo kuingia katika machafuko zaidi. Mamia ya wananchi vivyo hivyo nao wako upande wa jeshi.

Niger Protest in Niamey
Picha: AFP

Mkuu wa majeshi wa Niger Jenerali Abdou Sidikou Issa ametangaza kuunga mkono mapinduzi na kuongeza kwamba "kamanda ya kijeshi ya vikosi vya jeshi la Niger... imeamua kuunga mkono tamko la vikosi vya ulinzi na usalama ... ili kuepusha makabiliano mabaya kati ya vikosi mbali mbali". Taarifa hiyo inaarifu kuwa jeshi lilihitaji "kulinda uadilifu" wa rais na familia yake na kuepuka "makabiliano mabaya ... ambayo yanaweza kusababisha umwagaji damu na kuathiri usalama wa watu.

Kikosi maalum kilichofanya mapinduzi: Wanajeshi wa Niger wadai kumuondoa madarakani Rais Bazoum

Mamia ya wafuasi wa mapinduzi hayo walikusanyika mbele ya bunge la kitaifa mjini Niamey, wakipiga muziki wa kulisifu jeshi. Baadhi walipeperusha bendera za Urusi na kutoa kauli mbiu za kuipinga Ufaransa, zikiashiria kuongezeka kwa chuki dhidi ya mkoloni wa zamani na ushawishi wake katika eneo la Sahel. Baadhi yao wamesema kwamba "Tumepiga hatua. Mungu akipenda ndani ya mwezi mmoja, magaidi wote watarudi walipotoka. "

"Tunafikiri kwamba kinachohitajika leo ni kuwa na mshirika wa maslahi sawa, sio mshirika ambapo Magharibi pekee ndiyo hufaidika. Ni juu ya utu, ndio shida yetu."

Wafuasi wa mapinduzi ya kijeshi walipovamia makao makuu ya chama cha Rais Bazoum cha PNDS mjini NiameyPicha: AFP

Vijana wengine pia walifika katika makao makuu ya chama cha Bazoum cha PNDS, kukivamia na kuchoma moto baadhi ya magari.

Awali, wakati maafisa wa nchi za magharibi wakisema kuwa jaribio la mapinduzi hayo bado halikuwa wazi, Rais Bazoum na waziri wa mambo ya kigeni Hassoumi Massoudou, walipinga unyakuzi wa madaraka. Waziri wa mambo ya kigeni Massoudou amesisitiza kuachiliwa kwa Rais Bazoum na kuwataka viongozi wa mapinduzi kutatua madai yao kupitia njia ya mazungumzo. Haya ni mapinduzi ya saba katika kanda ya afrika Magharibi na kati tangu mwaka 2020. Bado haikuwa wazi nani haswa atachukua madaraka ya Bazoum. Kwa hivi sasa kikosi maalum cha walinzi wa rais kinaongozwa na Jenerali Omar Tchiani, lakini tamko la kuchukua madaraka lilitolewa na msemaji Kanali Meja Amadou Abramane.

Miito ya kulaani mapinduzi

Mkuu wa masuala ya haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Turk ameelezea kusikitishwa na kushangazwa na jaribio la mapinduzi ya kunyakua madaraka. Amesema juhudi zote zinapaswa kuchukuliwa ili kurejesha utulivu wa kikatiba na utawala wa sheria.

Soma pia: Jeshi la Niger latangaza rasmi mapinduzi dhidi ya Bazoum

Wakati huohuo pia, Urusi nayo imetoa tamko kuhusu yanayoendelea Niger. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje Maria Zakharova amesema "wanategemea jeshi kumwachilia haraka rais Bazoum na kuzitaka "pande zote katika mzozo huo kujizuia katika matumizi ya nguvu na kutatua migogoro yote kwa njia za amani na mazungumzo yenye tija".

Vyanzo: reuters/dpa/afp

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW