1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi nchini Myanmar lawaachia huru wafungwa 600

24 Machi 2021

Myanmar imewaachia huru zaidi ya wafungwa 600 waliokamatwa katika maandamano ya kupinga mapinduzi ya kijeshi pamoja na mpiga picha wa shirika la habari la Associated Press aliyekamatwa katika maandamano hayo

Myanmar Rangun | Festgenommene Demonstranten im Bus
Picha: AP Photo/picture alliance

Mamia ya watu waliokamatwa na kuhukumiwa kifungo gerezani  kwa kupinga mapinduzi ya mwezi uliopita nchini Myanmar leo wameachiwa huru katika ishara ya kwanza ya jeshi linaloonekana kujaribu kutuliza harakati za maandamano. Walioshuhudia tukio hilo nje ya Gereza la Insein mjini Yangon waliona mabasi mengi yakiwa yamejaa vijana, wakionekana wenye furaha na wengine wakionesha ishara ya vidole vitatu inayotumika kuonesha upinzani wao dhidi ya mapinduzi hayo. Kituo cha televisheni cha serikalikimesema kuwa jumla ya wafungwa 628 wameachiwa huru.

Afisa mmoja wa magereza ambaye alizungumza kwa sharti la kutotajwa, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba wamewaachia huru wanaume 360 na wanawake 268 kutoka gereza hilo la Insein. Wafungwa hao wanaonekana kuwa mamia ya wanafunzi waliowekwa kizuizini mapema mwezi Machi wakati wa maandamano dhidi ya mapinduzi ya Februari 1 yalioiondoa mamlakani serikali iliyochaguliwa kikatiba ya Aung San Suu Kyi.

Aung San Suu Kyi- Kiongozi wa Myanmar aliyepinduliwa madarakaniPicha: Athit Perawongmetha/REUTERS

Wakili mmoja ambaye pia alizungumza kwa sharti la kutotajwa jina kwa kutotaka kutambuliwa na mamlaka amesema kuwa wale wote walioachiwa huru walikamatwa mnamo Machi 3. Alisema ni watu 55 tu ambao wamesalia gerezani  na kuna uwezekano wakashtakiwa chini ya Kifungu cha 505 (A) cha Kanuni ya Adhabu, ambacho hubeba adhabu ya hadi miaka mitatu gerezani.

Miongoni mwa walioachiwa huru ni mwanahabari wa shirika la Assoiated Press Thein Zaw aliyekamatwa mwezi uliopita alipokuwa akifuatilia maandamano ya kupinga mapinduzi ya kijeshi nchini humo. Zaw aliliarifu shirika hilo na familia yake kuhusu kuachiwa huru kwake kwa njia  ya simu baada ya kikao cha pili cha kusikilizwa kwa kesi dhidi yake . Alisema kuwa jaji anayesimamia kesi yake alisema kuwa  mashtaka yote dhidi yake yameondolewa kwasababu alikuwa akifanya kazi yake alipokamatwa.

Katika taarifa, shirika la msaada la Save the Children, limesema kuwa kiasi cha watu 20 wa umri wa chini ya miaka 18 wameuawa katika msako wa polisi nchini humo na kwamba linahofu kuwa watoto wanaendelea kulengwa katika mashambulizi makali dhidi ya waandamanaji wa amani na kutoa wito kwa vikosi vya ulinzi kuhitimisha mara moja mashambulizi hayo.

Hii leo waandamanaji walijaribu mbinu mpya waliyoitaja kuwa mgomo wa kimya na kutoa wito kwa watu kubaki majumbani na shughuli zote kufungwa kwa leo.