Jeshi, waasi DRC 'wala nyama za watu'
4 Julai 2018Kundi hilo la watalaamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu wanaoendeleza uchunguzi katika eneo la Kasai linalokumbwa na mzozo wameliambia Baraza la Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu kuwa wanashuku pande zote nchini Congo zimehusika katika uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu.
Ripoti yao ya kina yenye kurasa 126 inaeleza mashambulizi ya kinyama yaliyofanywa katika jimbo la Kasai tangu mzozo kuzuka mwishoni mwa mwaka 2016,kati ya waasi wa kundi la Kamwina Nsapu na majeshi ya Congo.
Miongoni mwa ushahidi uliokusanywa unaeleza kuwa vijana wamelazimishwa kuwabaka mama zao, wasichana wadogo wamerubuniwa kuamini kuwa nguvu za kichawi zitawafanya kuwa na uwezo wa kushika risasi za moto na wanawake wamelazimishwa kuchagua kati ya kubakwa na magenge au kuuawa.
Waziri wa Masuala ya Haki za Binadamu wa Congo, Marie Ange Mushobekwa, ameliambia Baraza la Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu kuwa kile kinachojiri Kasai hata hakiwezi kuelezeka.
Ukatili usiosemeka
Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa inasema mmoja wa waathiriwa wa maovu yanayojiri Kasai aliwaeleza wachunguzi wa Umoja huo kuwa mnamo mwezi Mei mwaka jana, aliliona kundi la wapiganaji wa Kamwina Nsapu wakiwa na sehemu nyeti za wanawake wakizionesha kama medali.
Wanajeshi wa Congo wanadaiwa kuonekana wakiwakatakata watu, kupika viungo vyao vikiwemo sehemu nyeti za wanaume waliokatwa shemu zao za siri wakiwa hai au wengine wakiwa wamekufa na kuzila nyama hizo na kunywa damu.
Mchunguzi mkuu Bacre Waly Ndiaye ameliambia baraza hilo la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa kuwa katika tukio moja, takriban wanaume na vijana wa kiume 186 kutoka kijiji kimoja walikatwa vichwa na waasi wa Kamwina Nsapu, kundi ambalo wengi wa wapiganaji wake ni watoto waliolazimishwa kujiunga nalo.
Watoto hao wapiganaji ambao hawana silaha, wakiwa wamejihami tu na marungu na fimbo, wamerubuniwa kuamini kuwa wana nguvu zinazowakinga dhidi ya hatari.
Wengi wao wameuawa na wanajeshi wa serikali waliowamiminia risasi kiholela na baadaye miili kuzikwa katika makaburi ya watu wengi au miili yao kurundikwa katika lori za kijeshi na kwenda kuzikwa kwingineko.
Makaburi ya pamoja
Umoja wa Mataifa unaamini kuwa kuna mamia ya makaburi ambapo watu wengi wamezikwa kwa pamoja.
Afisa mmoja wa serikali ya Congo ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa taarifa hizo zilizokusanywa na wachunguzi zinapaswa kupitishwa kwa mahakimu wa nchi hiyo.
Afisa huyo amesema hawafahamu kuhusu madai hayo na wanaamini yamechochewa kisiasa na hayana chochote kuhusiana na suala la haki.
Mushobekwa amesema serikali imeshirikiana kikamilifu na wachunguzi hao wa Umoja wa Mataifa na inataka ukweli kudhihirika lakini ameongeza kusema baadhi ya yaliyomo kwenye ripoti hiyo yanatiliwa shaka kwani uchunguzi uliendeshwa haraka.
Waziri huyo wa masuala ya haki za binadamu Congo amesema kile ambacho ni bayana ni kuwa maafisa wa usalama waliotuhumiwa kuhusika na maovu, iwapo itabainika ni kweli, watawajibishwa kwa matendo yao na wataadhibiwa vikali.
Mwandishi: Caro Robi/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga