1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jimbo la Massachusetts laenda Republican

20 Januari 2010

Pigo kwa Rais Obama na bima ya afya.

Barack Obama (apata pigo)Picha: AP

USHINDI WA REPUBLICAN MASSACHUSETTS:

Chama cha upinzani cha Republican nchini Marekani ,kimejipatia ushindi mkubwa jana usiku kwa kukinyakua kiti cha Baraza la Senate cha jimbo la Massachuettts, ngome kubwa ya chama cha Democrat cha rais Barack Obama .Cha kustusha zaidi , ni kwamba pigo hilo limekuja siku ile ile rais Obama, anaadhimisha mwaka kamili tangu kutawazwa rais wa Marekani.

Mrepublican, Scott Brown, amezusha msangao huo kwa ushindi wake wa asilimia 52% dhidi ya 47% ya kura za bibi Martha Coakley wa chama cha Democrat.Matokeo ya uchaguzi huo ya kujaza kiti kilichoachwa wazi kwa kifo cha Seneta Edward Kennedy,y atazamiwa kuathiri mpango wa mageuzi ya bima ya afya wa rais Obamai.

KITI CHA AKINA KENNEDY KIMEPOTEA:

Kura takriban zote zikiwa zimehesabiwa, Scott Brown wa chama cha Republican, amelin'goa shina la chama cha Democratic huko Massachusetts na kumpa rais Barack Obama zawadi asioitazamia siku ya kutimizwa mwaka madarakani. Mtetezi wa Democratic party, Bibi Martha Coakley, awali alitazamia ushindi wazi kabisa, kwani, jimbo la Massachusetts ni lao tangu nusu karne iliopita kuanzia enzi za rais J.F Kennedy, hata nduguye, marehemu Edward Kennedy,aliefariki August mwaka jana, na kuacha kiti hicho wazi."Leo sauti huru za wafuasi wasioegemea chama chochote katika Massachusetts zimesikika." alisema, mshindi Scott Brown.

Bibi Coakley, kwa upande wake, alisema amevunjwa moyo na matokeo, lakini, aliongeza kusema "najua tutanyanyuka na kusimama wima kesho kuendelea na vita." Mtetezi huyo wa Democratic aliarifu kwamba, amempongeza Scott Brown, mpinzani wake.

Hata hivyo, pigo kubwa wanasema wachambuzi, limekwenda kwa rais Obama ambae akionesha kufuata nyayo za akina Kennedy na sasa amelipoteza jimbo lao.Pale Bw.Scott Brown ,atapokalia kiti chake katika Baraza la Senate, Wademocrat wataendelea kuwa na wingi wa kura, lakini watapoteza kura ya 60 itakayo waruhusu kuzima upinzani wa chama cha Republican juu ya ajenda yoyote ya Ikulu.

PIGO KWA OBAMA

Mateka wa kwanza , wanadai wachambuzi, ni mpango wa rais Obama wa mageuzi ya bima ya afya ambao ukiyumbayumba kupitishwa katika Congress-Bunge la Marekani, licha ya wingi wa kura za wademocrat.

Rais Obama amempongeza Bw.Scott kwa ushindi wake jana usiku na kwa kampeni nzuri alioiendesha.Kwa mujibu wa msemaji wa Ikulu (white House),Robert Gibbs, rais Obama amemuarifu Scott kuwa yuko tayari kushirikiana nae katika kukabiliana na changamoto kali za uchumi zinazozikabili familia za wakaazi wa Massachusetts na za familia za wa nynge kote nchini Marekani.Wafuasi wa seneta huyu mpya katika makao makuu yake makuu wakishangiria ushindi na kuueleza "ni miujiza."

Mwandishi: Ramadhan Ali/AFPE

Mhariri: Miraji Othman