1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jimbo la Wakurdi laandamwa baada ya kura ya maoni

Josephat Charo28 Septemba 2017

Safari za ndege kutoka ndani na nje ya jimbo la Kurdistan, Iraq zitasimamishwa kuanzia Ijumaa jioni, kwa amri iliyotoka Baghdad, baada ya kura ya maoni iliyokuwa na utata iliyowapa wakurdi haki ya kuunda taifa lao.

Irak Haider al-Abadi, Ministerpräsident
Picha: Reuters TV

Kulingana na Mkurugenzi wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Erbil Talar Faiq Sali, safari zote za ndege za kimataifa zitasimamishwa kuanzia saa kumi na mbili jioni siku ya Ijumaa kufuatia uamuzi uliotolewa na bunge la Iraq na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Haider al-Abadi. Waziri Mkuu Haider al Abadi alitoa amri hiyo kama adhabu baada ya kura ya maoni kufanyika siku ya Jumatatu licha ya Iraq kuipinga. Takriban asilimia 92.73 walisema ndio katika kura hiyo iliyotaka uhuru wa wakurdi.

Aidha ndege nyengine kutoka kanda ya Mashariki ya kati likiwemo shirika la ndege la Uturuki, Misri na Lebanon walikwishatangaza watasimamisha safari zao kuelekea Kurdistan kufuatia ombi kutoka kwa serikali ya Iraq.

Akizungumza na shirika la habari la AFP Talar Faiq Sali, Mkurugenzi wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Erbil amesema anasikitishwa na uamuzi huo, akiutaja kwamba utarejesha nyumba juhudi za kupambana na wanamgambo wa dola la kiislamu nchini Iraq na katika taifa jirani la Syria pamoja na hatua ya kupeleka misaada kwa wale waliyopoteza makaazi yao kufuatia mashambulizi yanayofanywa na kundi la dola la kiislamu, IS.

Shirika la ndege la Qatar nalo limesitisha safari zake Picha: picture alliance/dpa/epa/Stringer

Amesema kuna wakimbizi wengi wanaotumia uwanja huo wa ndege na kwamba unatumiwa pia kama daraja na Syria pamoja na Umoja wa Mataifa kufikisha misaada kwa watu wanaoihitaji. Bi Faiq Sali ameongeza kuwa uwanja huo wa ndege unatumia pia na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani kwa hiyo kuufunga au kusimamisha safari za ndege kuingia na kutoka katika uwanja huo kutamuathiri kila mtu na kwamba sio hatua nzuri iliyochukuwaliwa.

Shirika la ndege la Qatar pia limetangaza kusimamisha safari zake kuanzia tarehe 29 Septemba hadi Oktoba mosi.

Iraq inaendelea kuishinikiza Kurdistan kufuta matokeo ya kura ya maoni

Hapo jana Iraq iliiwawekea shinikizo wakurdi kuufutilia mbali matokeo ya kura ya maoni huku bunge likiihimiza serikali kuu kutuma vikosi vyake kuyadhibiti maeneo muhimu tajiri kwa mafuta, yanayoshikiliwa na vikosi vya kikurdi. Iraq kwa upande wake imeyataka mataifa jirani kukatisha operesheni zao za kidiplomasia katika mji mkuu wa Kurdistan Erbil.

Aidha kura hiyo ya maoni imeibua kitisho au hofu ya kutokea mgogoro mpya wa kikanda. Ujumbe wa kijeshi kutoka Iraq tayari unaelekea nchi jirani ya Iran kushirikiana kijeshi kama mkakati wa kulipiza kisasi unaochukuliwa na serikali ya Iraq kufuatia kura hiyo ya maoni.

Iran na Uturuki pia zinapinga hatua zozote za kujitenga kwa wakurdi na majeshi yao yameanza mafunzo ya pamoja mpakani mwa Kurdistan katika siku za hivi karibuni. Iraq na Uturuki pia wameanzisha vikosi vya kijeshi vya pamoja.

Mwandishi:  Amina Abubakar /AFP/AP

Mhariri: Josephat Charo