DW yamtunuku Jimmy Lai kwa kutetea uhuru wa habari
24 Juni 2026
Mjasiriamali wa vyombo vya habari na mtetezi wa demokrasia wa Hong Kong Jimmy Lai ametunukiwa Tuzo ya Uhuru wa Kujieleza ya Deutsche Welle (DW) mwaka huu kwa mchango wake katika kutetea uhuru wa habari na haki ya kujieleza.
Lai, mwenye umri wa miaka 78, kwa sasa anatumikia kifungo cha miaka 20 jela mjini Hong Kong baada ya kukutwa na hatia ya kile mamlaka zilichokiita "kushirikiana na nguvu za kigeni." Kesi yake imekuwa alama ya hali inayozidi kuzua wasiwasi kuhusu uhuru wa vyombo vya habari katika eneo hilo.
Tuzo hiyo ilitolewa Jumanne katika Kongamano la Kimataifa la Vyombo vya Habari la Deutsche Welle - Global Media Forum, linalofanyika mjini Bonn, Ujerumani.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Jodie Ginsberg, Mkurugenzi Mkuu wa Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari (CPJ), alisema Lai amekuwa mfano wa mtu aliyesimama kidete kutetea vyombo vya habari huru licha ya gharama kubwa binafsi.
Alisema mashambulizi dhidi ya gazeti la Apple Daily na vyombo vingine vya habari vya Hong Kong yalitangulia hatua kubwa zaidi za kubana uhuru wa kiraia zilizofuata katika miaka ya karibuni.
Kutoka mhamiaji maskini hadi tajiri wa vyombo vya habari
Safari ya Jimmy Lai ilianza akiwa mtoto wa miaka 12 aliyekimbia kutoka Guangzhou kusini mwa China kuelekea Hong Kong, iliyokuwa koloni la Uingereza wakati huo.
Akiwa hana chochote, Lai alijijengea utajiri kupitia biashara ya nguo na mwaka 1981 akaanzisha chapa maarufu ya Giordano, ambayo ilimfanya kuwa mmoja wa wafanyabiashara wenye mafanikio makubwa Hong Kong.
Hata hivyo, tukio la mauaji ya waandamanaji waliokuwa wanadai demokrasia katika Uwanja wa Tiananmen mjini Beijing mwaka 1989 lilibadilisha kabisa mtazamo wake kuhusu siasa na uhuru.
Baada ya hapo, aliamua kutumia sehemu ya utajiri wake kuunga mkono harakati za demokrasia na kuingia katika sekta ya vyombo vya habari.
Alianzisha Jarida la Next na baadaye gazeti la Apple Daily, ambalo lilijulikana kwa uchunguzi wa kina, ukosoaji wa serikali na kuunga mkono waziwazi harakati za demokrasia Hong Kong.
Sauti ya demokrasia Hong Kong
Kwa miaka mingi, Apple Daily lilikuwa moja ya vyombo vya habari vyenye ushawishi mkubwa Hong Kong.
Gazeti hilo lilichanganya habari za uchunguzi, biashara, burudani na siasa, huku likibaki kuwa jukwaa muhimu kwa sauti zinazoikosoa Beijing.
Lai mwenyewe alishiriki katika maandamano makubwa ya harakati za Vuguvugu la Miavuli la mwaka 2014 na maandamano ya kupinga sheria ya kurejesha washukiwa China mwaka 2019.
Baada ya Beijing kuweka Sheria ya Usalama wa Taifa mwaka 2020, Lai alikamatwa na Apple Daily kulazimika kusitisha shughuli zake mwaka mmoja baadaye.
Tangu wakati huo, vyombo vingine kadhaa vya habari vinavyojitegemea pia vimefungwa au kusitisha shughuli kutokana na mazingira yanayozidi kuwa magumu kwa uhuru wa habari.
Miaka zaidi ya mitano gerezani
Jimmy Lai amekuwa gerezani tangu Desemba mwaka 2020 na amekaa zaidi ya siku 2,000 katika mazingira ya kutengwa.
Mnamo Februari mwaka huu alihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela, adhabu inayochukuliwa kuwa mojawapo ya kali zaidi kutolewa chini ya Sheria ya Usalama wa Taifa.
Mahakama ilisema Lai alitumia ushawishi wake na gazeti la Apple Daily kupinga mamlaka ya Chama cha Kikomunisti cha China na serikali ya Hong Kong.
Lai alikana mashtaka yote dhidi yake, lakini timu yake ya wanasheria imesema hatakata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.
Familia yake imeeleza wasiwasi mkubwa kuhusu afya yake, ikisema ana ugonjwa wa kisukari na amepungua uzito kwa kiasi kikubwa akiwa gerezani.
Tuzo yenye ujumbe wa mshikamano
Mwanawe, Claire Lai, ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kampeni za kutaka aachiliwe huru, amesema tuzo hiyo ina umuhimu mkubwa kwa familia yao.
Kulingana naye, tuzo hiyo inathibitisha kuwa wale wanaopigania uhuru wa wengine hawasahauliki hata wanapokabiliwa na mateso.
"Watu wanaopigania uhuru, na wale wanaopigania uhuru wa wengine, kamwe hawako peke yao," alisema katika mahojiano na DW.
Claire alisema anaamini baba yake angefurahi sana kujua kwamba ametunukiwa tuzo hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa DW Barbara Massing alisema taasisi hiyo inamtambua Jimmy Lai kwa kujitolea kwake kusikoyumba katika kutetea maadili ya kidemokrasia na uhuru wa habari.
Je, kuna siku ataachiwa huru?
Swali kubwa linalobaki ni kama Jimmy Lai ataweza kutoka gerezani akiwa hai. Familia yake inasema imepita miaka mitano tangu wamwone ana kwa ana, huku mawasiliano yao yakifanyika kwa njia ya barua pekee.
Sebastien Lai alisema mojawapo ya ndoto zake kubwa ni siku ambayo baba yake atarudi nyumbani na familia yote kukaa pamoja mezani kwa mara nyingine.
Hata hivyo, matumaini hayo yanaendelea kufifia kadiri miaka inavyosonga mbele.
Kwa wengi, Jimmy Lai amekuwa zaidi ya mfungwa wa kisiasa; amegeuka kuwa ishara ya mapambano ya uhuru wa habari, demokrasia na haki ya wananchi kupata taarifa bila hofu ya ukandamizaji.