1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin anaulaumu uongozi wa Sovieti kwa ujinga

1 Novemba 2019

Wakati Ukuta wa Berlin ulipoanguka, serikali ya iliyokuwa Umoja wa kisovieti ilirudi nyuma na kuiacha serikali ya Kikomunisti ya Ujerumani Mashariki kuporomoka. Rais wa Urusi sasa anaulaumu uongozi wa Sovieti kwa ujinga

Symbolbild Kommunismus
Picha: Fotolia/Savenko Tatyana

Warusi wengi wana mtazamo sawa unaoiangalia hatua ya kuporomoka kwa ukuta wa Berlin na kuungana tena kwa Ujerumani kama wakati ambao Urusi ilizijongelea nchi za Magharibi ikitumai kuanza enzi mpya ya ushirikiana lakini ilidanganywa na nchi zenye nguvu za Magharibi.

Rais wa iliyokuwa Usovieti Mikhail Gorbachev aliwatia shime viongozi wa kikomunisti katika ulaya ya Kati na Mashariki kufuata mfano wake katika kuanzisha mageuzi ya kiliberali na kutochukua hatua za kuzifikisha ukingoni serikali zao wakati zilipoanza  kuporomoka kufuatia mashinikizo ya makundi ya wanaounga mkono demokrasia.

Katika mwaka 1989 wanamageuzi waliichukua madaraka kote kwenye nchi  zilizokuwa chini ya Umoja wa kisovieti na kuumaliza utawala wa kikomunisti uliokuwa umedumu kwa zaidi ya miongo minne. Kwa Gorbachev binafsi  mabadiliko hayo yaliyofanyika kiwepesi kabisa yalikuwa ya ghafla kwake.

Kiongozi huyo wa zamani wa Sovieti aliwahi kusema katika mahojiano ya hivi karibuni kabla ya kuelekea kumbukumbu ya  miaka 30 ya kuanguka kwa ukuta wa Berlin Novemba tisa, kwamba aliyakaribisha mageuzi ya kidemokrasia katika Ujerumani Mashariki na katika nchi nyinginezo zilizokuwa kwenye Umoja wa Kisovieti lakini hakufikiria kwamba ukuta wa Berlin ungeporomoka haraka kama ilivyotokea.

Michael GorbatschovPicha: picture-alliance/dpa/A. Scheidemann

Gorbachev aliliambia gazeti la Izvestia kwamba sio tu Wasovieti lakini hata washirika wao wa nchi za Magharibi hawakutarajia kwamba  historia ingewekwa kwa kasi kubwa kama ilivyotokea  ilivyotokea.

Asubuhi ya baada ya kuangushwa ukuta wa Berlin, Gorbachev aliitisha kikao na chama tawala cha kikomunisti Politburo kujadili hatua itakayochukuliwa na Sovieti. Gorbachev anasema,chama hicho kiliamua kwa kauli moja kuondowa kabisa uwezekano wa kutumiwa nguvu kujibu hatua hiyo.

Baadhi bila shaka walikuwa na hamu ya kurudisha sheria kwa kutumia vifaru,lakini wote walikaa kimya wakati huo alisema Gorbachev. Pavel Palazchchenko ambaye alikuwa ni mkalimani wa Gorbachev wakati huo anasema kwamba hatua yoyote ya aina nyingine ingeweza kuwa athari mbaya kabisa na pengine ingelikuwa ni mwanzo wa kuzuka janga.

Umoja wa kisovieti ulikuwa na wanajeshi 300,000 na zaidi ya vifaru 12,000 na magari mengine ya kijeshi katika Ujerumani Mashariki.Vladislav Zubok mtaalamu kuhusu historia ya Sovieti katika chuo cha uchumi cha London Uingereza anasemakimsingi Umoja wa kisovieti ungeweza kuufunga mpaka wote kwa kutumia vifaru vyao lakini waliamua kubakia kwenye kambi zao.

Ilikuwa wazi kwa uongozi wa Sovieti kwamba ilikuwa haiwezekani tena kuyazowa maji ambayo yameshamwagika. Na enzi mpya zikaanza. Nikolai Andreyev ambaye alikuwa kanali wa kijeshi Mashariki mwa Ujerumani anasema alishusha pumzi kuona uongozi wa Kisovieti haukujaribu kupigania kuwa na udhibiti wa eneo hilo kwa kutumia nguvu.

Lakini mpaka leo warusi wengi akiwemo rais Vladmir Putin wanaendelea kumtwika dhamana Gorbachev kwa kuwahujumu washirika wake wa Kisovieti Ujerumani Mashariki  na maslahi muhimu ya Urusi katika mazungumzo na nchi zenye nguvu za Magharibi.