Shambulio la Magdeburg linavyochochea mrengo mkali Ujerumani
24 Desemba 2024Lengo la Talib A., mtuhumiwa wa shambulio hilo la soko la Krismasi mjini Magdeburg, bado halijulikani wazi. Kilichothibitishwa ni kwamba yeye ni raia wa Saudi Arabia na yuko kizuizini.
Hata hivyo, mara baada ya shambulio hilo, wafuasi wa mrengo wa kulia nchini Ujerumani walianza kuwachokoza wahamiaji.
"Sijawahi kushuhudia mazingira yenye chuki na vitisho vya kiwango hiki,” alisema mwanafunzi anayesomea uhandisi wa magari huko Magdeburg, mji mkuu wa jimbo la Saxony-Anhalt.
Kituo cha kuzuia vurugu cha Salam, kilichopo Saxony-Anhalt, pia kilitoa maelezo yanayofanana. Chama hicho kimeripoti ongezeko kubwa la matukio dhidi ya watu wanaoonekana kama wageni kwa mtazamo wa wafuasi wa mrengo wa kulia.
Soma pia: Ujerumani yachunguza maonyo kuhusu muuaji wa soko la Krismas
Kwa mujibu wa Salam, "wahamiaji wanaoonekana wanaitwa 'magaidi,' 'wahalifu' na 'watu wasio na maadili,' baadhi yao wanasukumwa na kutemewa mate."
Vitisho hivyo vimefikia kiwango ambacho jamii za wahamiaji zimeanza kuonyana kupitia makundi ya WhatsApp na Facebook kutotembea katika maeneo ya wazi.
Kwamba mtuhumiwa wa shambulio la Magdeburg anashukiwa kuwa mwenye chuki dhidi ya Uislamu na mfuasi wa mrengo mkali wa kulia ni jambo lenye utata, alisema Hans Goldenbaum, mtaalamu wa masuala ya itikadi kali kutoka Salam, alipokuwa akizungumza na chombo cha habari cha MDR cha Ujerumani.
"Hii inaonyesha nguvu ya simulizi za mrengo mkali wa kulia na jinsi zilivyojitenga na uhalisia."
Uhamasishaji wa kitaifa ya wafuasi wa mrengo mkali wa kulia
Tangu shambulio hilo la soko la Krismasi, wafuasi wa mrengo mkali wa kulia na wanazi mamboleo, vyama, na watu binafsi wamehamasika kote Ujerumani. Wanadai wahamiaji wote wafukuzwe nchini.
Mamia ya wanazi mamboleo walikusanyika kwenye maandamano ya mrengo wa kulia huko Magdeburg Jumapili, siku mbili baada ya shambulio hilo. Maandamano hayo yalishuhudia mashambulizi dhidi ya waandishi wa habari.
Mmoja wa wazungumzaji kwenye maandamano hayo alikuwa Thorsten Heise. Mnazi huyo Mamboleo mwenye itikadi kali ana hatia ya makosa kadhaa ya jinai. Aliwahi kujaribu kumgonga mkimbizi kwa gari lake. Video za maandamano hayo zinaonyesha Heise akiwahimiza waandamanaji kujiingiza katika vyama, idara za zimamoto, na mamlaka mbalimbali.
Waandishi wa habari na waangalizi waliripoti kuwa washiriki wa maandamano walikuwa wakipaza sauti wakisema "Amka Ujerumani," kauli iliyotumiwa wakati wa utawala wa Wanazi chini ya Adolf Hitler. Matumizi ya kauli hiyo ni kosa la jinai nchini Ujerumani.
Soma pia: Ujerumani: Gari laparamia watu soko la Krismasi mjini Magdeburg
Kulingana na makadirio ya polisi, hadi watu 3,500 - wakiwemo viongozi wa vyama na wafuasi wa itikadi kali kutoka kundi la vurugu za mpira wa miguu - walihudhuria maandamano yaliyoandaliwa na chama cha mrengo mkali wa kulia cha Alternative for Germany (AfD). Mavazi na tattoo zilizojulikana miongoni mwa wafuasi wa ubaguzi wa rangi zilionekana wazi.
Kiongozi wa AfD, Alice Weidel, alipokuwa akihutubia, umati ulipiga kelele: "Fukuza, fukuza, fukuza." Baada ya maandamano hayo, washiriki walijitokeza mitaani, wakawashambulia wapiga picha, wakapaza kauli za utaifa, na kupima nguvu za polisi waliokuwa wakiwafuatilia.
Siasa zimeanza kujihusisha na shambulio hilo
David Begrich, mtaalamu wa itikadi kali za mrengo wa kulia kutoka chama cha Miteinander mjini Magdeburg, anatarajia kwamba shambulio la soko la Krismasi litaendelea kupewa uzito wa kisiasa.
Chama cha AfD kimeandaa maandamano makubwa huko Magdeburg. Begrich alikosoa vikali maandamano hayo, akisema kwamba baada ya shambulio hilo, nashari inapaswa kubaki kwa waathiriwa watano na wengine 200 waliojeruhiwa.
Soma pia:Hotuba ya Krismasi: Rais wa Ujerumani atoa wito wa umoja
"Ninashuhudia mshangao mkubwa na mshtuko huko Magdeburg,” aliiambia DW. "Shambulio hili limeuumiza sana mji huu. Hii pia inanihusu binafsi: mke wangu alikuwa mmoja wa waliojeruhiwa.”
Begrich alisema anaamini kwamba hakuna anayepaswa kulihusisha shambulio hilo na siasa wakati bado kuna waathiriwa hospitalini: "Mambo ya waathiriwa yanapaswa kuwa kipaumbele cha kwanza. Marekebisho yanakuja baadaye. Jamii hazitaki masuala ya kisiasa kuingilia.”
Licha ya taarifa za uongo, uvumi, na juhudi za kisiasa za kulihusisha shambulio hilo kwenye mitandao ya kijamii, Begrich anahisi mji wake umeathirika sana: "Mji unakuja pamoja.”