1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jinsi Ujerumani inavyotafuta kupunguza gharama za umeme

12 Januari 2025

Umeme ni ghali zaidi nchini Ujerumani kuliko sehemu nyingine yoyote barani Ulaya, hali inayowaathiri sana watumiaji katikati mwa mdororo wa kiuchumi. Wanasiasa wanatafuta suluhisho, lakini ni chaguo gani wanazo?

Ujerumani Wind turbine mbele ya mtambo wa nishati ya makaa ya mawe wa Neurath
Mnamo 2024, asilimia 59 ya umeme wa Ujerumani ulitoka kwa upepo, jua na nishati zingine zinazoweza kurejeshwa.Picha: Ina Fassbender/AFP/Getty Images

Mwaka mpya ulianza kwa hali ya hewa yenye dhoruba. Mitambo ya upepo ilikuwa ikifanya kazi kwa kasi kubwa huku jua liking'aa katika sehemu nyingi za nchi.

Matokeo yake ni kwamba uzalishaji wa umeme utokanao na nishati jadidifu ulichangia asilimia 125 ya mahitaji ya umeme nchini Ujerumani, kulingana na Taasisi ya Mifumo ya Nishati ya Jua ya Fraunhofer. 

Ugavi huu uliyopitiliza ulisababisha bei ya umeme kushuka kwenye masoko ya umeme, ambako bei huamuliwa na usambazaji na mahitaji, na kwa saa kadhaa umeme ulikuwa unapatikana bure. 

Mnamo 2024, wastani wa asilimia 59 ya umeme wa Ujerumani ulizalishwa kutoka kwenyd vyanzo jadidifu. Hata hivyo, wakati wa kipindi cha baridi chenye giza, uzalishaji huu haukuwa wa kutosha.

Soma pia: Ujerumani kufanya biashara ya nishati na Nigeria

Desemba 12, 2024, iliashiria kiwango cha chini zaidi, ambapo ni asilimia 18 pekee ya mahitaji ya umeme yalitimizwa kutokana na vyanzo vya nishati jadidifu.

Ujerumani inawekeza sana katika nishati mbadala na inabuni njia za kuhifadhi nishati ili kufidia wakati upepo au nishati ya jua ni ndogo.Picha: Sean Gallup/Getty Images

Umeme uliobaki ulizalishwa kutoka kwenye mitambo ya makaa ya mawe na gesi, pamoja na uagizaji wa umeme kutoka nchi jirani za Umoja wa Ulaya (EU). 

EU ina soko la umeme la pamoja, ambalo lina maana kwamba wakati wa upepo mkali na mwangaza wa jua, Ujerumani inaweza kuuza umeme nje, lakini wakati wa upungufu wa upepo na jua, huwalazimu kuagiza umeme zaidi.

Umeme mwingi ambao Ujerumani ilinunua mnamo 2024 ulitoka Ufaransa, ambayo inakidhi asilimia 70 ya mahitaji yake ya nishati kupitia nyuklia inayopatikana mwaka mzima. 

Uingizaji na usafirishaji wa umeme unategemea bei za wakati huo kwenye Soko la Nishati la Ulaya. Zaidi ya hayo, watumiaji wanapaswa kulipa kodi za kitaifa na ada.

Nchini Ujerumani, karibu asilimia 30 ya bei ya umeme inajumuisha gharama za mtandao wa umeme, ambazo ni gharama za kupanua mtandao huo. Kodi na ada zinachukua karibu theluthi nyingine ya bei hiyo. 

Bei za umeme kwa kaya na makampuni 

Kaya na makampuni kwa kiasi kikubwa hawajapata athari za moja kwa moja za mabadiliko ya bei kwa sababu mara nyingi wana mikataba ya muda mrefu ya umeme. Wanawalipa wasambazaji wa umeme bei iliyowekwa kwa kipindi maalum, kama ilivyoafikiwa kwenye mikataba. 

Soma pia: Ujerumani na India kushirikiana kulinda mazingira

Hata hivyo, tangu mwanzo wa mwaka 2025, wasambazaji wamewajibika pia kutoa viwango vya bei vinavyobadilika kulingana na bei za sasa. Kwa njia hii, wateja wanaotumia umeme mwingi, kama vile kwa kuchaji magari ya umeme au kuendesha pampu za joto, wanapewa motisha ya kifedha kupanga matumizi yao wakati ambapo umeme unapatikana kwa wingi na bei ni ya chini. 

Ujerumani ilifunga mitambo yake ya mwisho mwaka 2023.Picha: Michael Probst/AP Photo/picture alliance

Mnamo 2024, uzalishaji wa umeme kutokana na makaa ya mawe ulipungua kwa asilimia 8 nchini Ujerumani, huku makaa ya mawe meusi yakipungua kwa zaidi ya asilimia 27. Tangu 2015, asilimia ya umeme unaozalishwa kutoka makaa ya mawe imepungua kwa karibu nusu, na hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa CO2. 

Mwaka 2024 pia ulikuwa wa kwanza ambapo Ujerumani ilihitimisha uzalishaji wa umeme wa nyuklia wa ndani. Mitambo mitatu ya mwisho ya nyuklia, ambayo ilifungwa mnamo 2023, ilikuwa inachangia asilimia 6 ya uzalishaji wa umeme. 

Lakini je, ni upungufu wa nguvu za upepo na jua unaosababisha kupanda kwa bei? Au makampuni ya nishati yanaweza kuwa yanapandisha bei kimakusudi kwa kutoiunganisha mitambo yote ya makaa ya mawe na gesi kwenye mtandao ili kupunguza upatikanaji wa umeme?

Swali hili ndilo linachunguzwa sasa na Ofisi ya Ushindani ya Shirikisho la Ujerumani, ambayo ni sehemu ya Wizara ya Uchumi na iliyo jukumu la kuhakikisha ushindani wa haki sokoni. Ikiwa itagundua upangaji wa bei haramu, inaweza kutoza faini. 

Uchumi na bei za umeme 

Hakuna mahali barani Ulaya ambapo umeme ni ghali zaidi kuliko Ujerumani. Kulingana na Ofisi ya Takwimu ya Shirikisho, familia ya watu watatu hadi wanne ililazimika kulipa chini ya senti 40 kwa kilowati-saa mnamo 2024. Nchini Hungary na Bulgaria, ambako serikali hutoa ruzuku kwa umeme, watumiaji walilipa senti 10 pekee kwa kilowati-saa. 

Ujerumani pia ina ruzuku, lakini ni kwa ajili ya makampuni ya viwanda pekee. Hata hivyo, makampuni yanayotumia nishati nyingi yamekuwa yakilalamika kuwa gharama za nishati bado ni kubwa mno kwao kushindana kikamilifu. 

Wakati viwanda vilikuwa bado vinapata umeme kwa senti 12 kwa kilowati-saa mnamo 2021, bei ilipanda zaidi ya senti 50 mnamo 2022 kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Mnamo Julai 1, 2022, kodi na ada zilipunguzwa kwa kiasi kikubwa kwa makampuni. 

Ujerumani kupunguza tozo ya gesi asilia

01:21

This browser does not support the video element.

Leo, makampuni ya viwanda yanalipa takriban senti 17. Hata hivyo, hii bado ni zaidi ya kile ambacho makampuni yanalipa katika nchi nyingine kubwa za washindani.

Soma pia: COP27: Mataifa makubwa yaunda muungano wa nishati ya upepo

Mnamo 2023, kwa mfano, makampuni ya sekta ya magari nchini Ujerumani yalilipa zaidi ya mara mbili ya bei ya umeme ikilinganishwa na washindani wao nchini China na karibu mara tatu ya gharama za makampuni yanayolingana nchini Marekani.

Kupunguza kwa kiasi kikubwa bei za umeme bado ni mojawapo ya changamoto kubwa za kiuchumi. 

Muungano wa mrengo wa kulia wa vyama vya Christian Democratic Union (CDU) na Christian Social Union (CSU), ukiwa na Friedrich Merz kama mgombea wa ukansela, umetangaza katika ilani yao ya uchaguzi kwamba wanataka kupunguza ada za mtandao kwa nusu na kupunguza zaidi kodi ya umeme kwa makampuni yanayotumia nishati nyingi. Hata hivyo, haijabainika wazi jinsi hatua hii itakavyofadhiliwa. 

Kinachobaki wazi ni kwamba upanuzi endelevu wa nishati jadidifu, mitandao ya umeme, na vituo vya kuhifadhi nishati utaendelea kuwa ghali kwa miaka mingi ijayo. Ni baada ya miundombinu kukamilika ndipo faida za kifedha za upepo na nishati ya jua zitaanza kuonekana. 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW