Jinsi ukimwi unavyoathiri maisha ya watoto barani Afrika
1 Desemba 2005Maradhi ya ukimwi watu wamekua wakiyaangalia kama maradhi yanayowakumba watu wazima tuu.Na hata makampuni ya madawa hadi hivi karibuni yalikua yakitengeneza madawa kwaajili ya watu wazima tuu.Watoto waalisahauliwa kabisa katika vita dhidi ya ukimwi,licha ya kwamba idadi ya wanaoambukizwa inazidi kuongezeka.Watoto wachanga tisaa kati ya kumi walioambukizwa virusi vya ukimwi wanaishi barani Afrika.Kila mtu wa sita anaefariki mkwa ukimwi ni mtoto ndogo.Makampuni ya madawa ndio kwanza yameanza kuzindukana na kutengeneza madawa kwaajili yao.Ni nchi chache tuu zinazoinukia zinazoweza kumudu kununua madawa hayo.Nchini Afrika kusini watoto 50.000 wanahitaji dawa za ukimwi,lakini watoto elfu tano tuu ndio wanaopata dawa hizo.Nchi ndogo ya kifalme – Lesotho,inayokamata nafasi ya tatu ya nchi zenye wakaazi wengi walioambukizwa na maradhi ya ukimwi,ndio kwanza imeanza kuwahudumia watoto madawa ya ukimwi.Tebello ni mmoja wao.Wazee wake wote wawili wameambukizwa vijidudu vya HIV,na kwa karibu nusu mwaka sasa,familia nzima wameanza kutumia madawa ya kupunguza madhara ya ukimwi.
Hali katika kliniki ya wagonjwa wa ukimwi ya TSEPONG huko Leribe,kijiji chenye wakaazi laki mmoja na 60 elfu mtu anaweza kuitaja kua ni ya kawaida tuu.Unakuta watu waliokondeana,bwana mmoja ambae miguu yake imesalia mifupa tuu amekaa katika kigari cha walemavu,bibi mmoja ambae uso wake umesalia ngozi tuu na mafupa- licha ya yote hayo,wote wanavunja miko na kuzungumzia suala la ukimwi.Wote wamo ndani ya jahazi moja.Manyane MOTOBOLI ana umri wa miaka 39 na ndio kwanza amekwenda kuchukua dawa.Fungu lake la mwezi pamoja na binti yake wa miaka sita.Hapa tunazungumza lakini nyumbani hakuna anaejua hata watoto wetu wawili wa kike hawajui ,anasema,tunanukuu:
„Mume wangu daima amekua akisema nisiwaambie watoto chochote.Hata familia,si yake wala si yangu hakuna anaejua.Yeye tuu na mie na kakaangu ,tena kwasababu yeye ni muuguzi,ndio tunaojua.“
Manyane amearifiwa tangu may iliyopita kwamba mumewe na binti yake kitindamimba wameambukizwa virusi vya ukimwi.Mumewe alikua akifanya kazi katika migodi nchini Afrika kusini na alikua akija baadhi ya wakati tuu nyumbani,hadi aliposhikwa na ugonjwa,akikurubia kuiaga dunia.Ndipo alipofanikiwa kumshawishi akubali kupimwa,yeye na binti yao wa miaka sita –Tebello kuona kama hawajaambukizwa.
„Mtoto wetu huyu hajakua vizuri tangu alipozaliwa.Machozi yamekua yakimtoka na mafua kumtiririka na mwili wake mzima ni mdichi kupita kiasi-„ Anasimulia bibi Manyanne Motoboli.
Wote watatu,baba,mama na mtoto wa kike wa miaka 6 wameshikwa na virusi vya ukimwi.Wazee wanatumia madawa ya kupunguza madhara na tabello anapewa dawa za antibiotik ili aqweze kujikinga asiambukizwe na kwa namna hiyo pia urefushwe muda wa kumpatia madawa ya ukimwi.
Tangu Tebello alipoanza kumeza madawa,akaanza kuangalia televisheni na kucheza na wenzake nje.Msichana huyo wa miaka sita Tebello si tena mtoto aliyejiinamia,aliyechoka na dhaifu.Badala yake amekua mchezi,anahadithia na anapenda kwenda shule.
Anapenda kumeza vidonge vyake,kwasababu vinamsaidia pia dhidi ya homa ya mafua aliyo nayo.Mamaake anacheka tuu,kwasababu Tebello hajui kwanini anabidi kila wakati kumeza madawa.Mannyane angependelea sana kuwaeleza wanawe yaliyotokea-lakini aibu ni kubwa-hata kama mtaani kwao watu dazeni kadhaa wanakufa kila wiki-viunga vya makaburi vimejaa na hata idadi ya watoto wanaofariki dunia inazidi kuongezeka-kwasababu bila ya madawa,nusu tuu ya watoto walioambukizwa na virusi vya ukimwi ndio wanaoweza kupindukia umri wa miaka miwili.
Tangu miezi michache hivi kuna madawa ya kunywa ili kupunguza madhara ya ukimwi kwa watoto.Hapo awali watoto walikua wakifa kwasababu madaktari hawakua na maarifa ya kutosha katika kugawa madawa ya watuwazima kulingana na vipimo vya watoto.
Daktari Limpho Lekena anasema
„Watu walikua wakifikiri ukimwi ni maradhi ya watu wazima tuu,hayawashiki watoto.Katika kliniki hii tuna watoto 250 walioambukizwa virusi vya HIv na 80 kati yao wanameza dawa.
Unajikusanyia maarifa mengi tuu unapowauguza watoto.Wanachangamka haraka.Na wala hawafichi kitu.Wanakuja kliniki na kusema:nnajisikia vizuri.Wanaonekana pia vizuri na wanapata mwili haraka kuliko watu wazima.Na dalili zinatoweka haraka pia.Mtoto ambae awali alikua hata kwenda hawezi,utamuona mara anaanza kutembea na anaendelea pia vizuri.Na kama walikua hawendi shule,basi wanaanza tena kwenda shule wakipata matibabu.Inatia moyo kweli kweli.