1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jinsi wanawake walivyogeuzwa shabaha ya wapiganaji Kongo

22 Novemba 2022

Mashirika ya kutetea wanawake mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inaonya juu ya ongezeko la visa vya ukatili dhidi ya wanawake tangu kulipozuka upya vita kati ya jeshi la nchi hiyo na waasi wa kundi la M23.

Afrika DR Kongo Kayembe Camp
Picha: GUERCHOM NDEBO AFP via Getty Images

Familia ya Bibi Rosine Mwambutsa ni miongoni mwa watu zaidi ya 20,000 ambao walikimbia mapigano yaliyozuka baina ya jeshi la Kongo na kundi la waasi wa M23. Lakini sasa waasi hao wanazidi kusonga mbele katika maeneo kadhaa mkoani Kivu Kaskazini.

Bi Rosine aliyepewa hifadhi katika kambi ya wakimbizi nje kidogo na mji wa Goma aliiambia DW kwamba wanawake ndio hasa waliokuwa wanaandamwa. "Mara nyingi tunajiuliza wenzetu wanapotelea wapi. Wengine wanakwenda kutafuta kuni msituni na hawarudi tena. Wanakamatwa huko huko!"

Wakimbizi wa ndani wahitaji misaada Kongo

02:19

This browser does not support the video element.

Mashirika ya kutetea wanawake yalisema idadi ya wanawake wanaoendelea kudhalilishwa kingono pamoja na visa vingine vya ukatili imeongezeka tofauti na miaka miwili iliyopita katika eneo la mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Wanawake katika wilaya za Beni na Rutshuru wamelazimika kuyahama makaazi yao, hali inayowaathiri pakubwa katika juhudi za kusonga mbele kimaendeleo. 

"Hatuko huru kutembea. Ukitoka, njiani unakutana na watu wabaya. Wanachinja, wanabaka. Tunateswa sana. Tokea vita vianze hadi sasa, mwanamke wa Kikongamani anateseka kabisa." Alisema Kavugho Maliro kutoka wilaya ya Beni.

Mauaji dhidi ya wanawake

Mwanamke akiwa amesimama kwenye kambi ya wakimbizi ya ndani ya Kayembe, mashariki mwa Kongo.Picha: GUERCHOM NDEBO AFP via Getty Images

Katika mji wa Goma, mbali kidogo na maeneo ya mapigano, unyanyasaji dhidi ya wanawake pia umekuwa tatizo kubwa.

Zaidi ya wanawake watano walishuhudiwa kunyongwa na watu wasiofahamika katika kipindi cha wiki mbili, jambo ambalo limekuwa tishio kubwa kwa maisha ya wanawake, wakiwemo wasichana wanaofanya shughuli za usiku wanaolengwa na magenge ya watu.

"Kinachoniumiza sana ni kuona kuwa watu wamekuwa wanyama kabisa. Unaona wanamkamata mwanamke hadharani na wanamtendea matendo mabaya hapo hapo." Alisema Gislaine Neema kutoka kundi la Wanawake Jasiri mjini Goma.

Visa vya ukatili dhidi ya wanawake na wasichana vimekithiri katika mataifa mbalimbali ulimwenguni, lakini mashariki mwa Kongo, eneo ambalo linayumbishwa na vita kati ya jeshi la nchi hiyo na makundi ya waasi - yakiwemo M23 na ADF-NALU - hali imezidi kuwa mbaya.

Imeandikwa na Benjamin Kasembe/DW Goma
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW