1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jinsi ya kuzuia tembo kwenye mazingira

4 Juni 2020

Kumekuwa na ripoti kadhaa za mashamba ya watu Afrika Mashariki kuvamiwa na tembo. Lakini kuna mbinu mbalimbali unazoweza kufuata kuzuia wanyama hao wasiharibu mazingira yako, mazao yako au hata kutishia maisha yako.

Tembo wakitembea
Picha: picture alliance/dpa

Otesha pilipili katika bustani na mashamba

Tembo hawapendi pilipili kabisa. Na hivyo wakijua kwamba kuna hatari ya wao kula pilipili wanapokula mazao katika shamba fulani, huwa wanajaribu kuepuka shamba hilo. Unaweza pia kutumia pilipili kwa namna hizi kufukuza tembo:

Picha: DW/M. Mamun

- Changanya pilipili na mafuta ya injini yaliyotumika. Paka mchanganyiko huo kwenye kamba na kisha zifunge kuzunguka shamba lako ama bustani yako.

- Kusanya kinyesi cha tembo, weka pilipili juu yake na kisha washa mchanganyiko huo moto. Moshi utakaotokea utakuwa na harufu ya pilipili itakayowafukuza tembo.

- Tumbaku ikisagwa kisha ikachanganywa na mafuta ya injini na pilipili na kupakwa kwenye kamba zinazozunguka shamba ama bustani inaweza pia kufukuza tembo. Hata vumbi la tumbaku kutoka kwenye kiwanda cha tumbaku huweza kutumika bila kuchanganywa na pilipili.

Taarifa zaidi: Mataifa kuzuia usafirishaji wa tembo mijini na kwenye 'zoo'

Tumia taa zenye mwanga mkali

Picha: picture-alliance/dpa/G. Herbert

Unaweza kuweka taa zitakazowaka kwa mwanga mkali sana mara tembo wanapotokea. Taa hizo zitawaogopesha tembo.

- Taa lazima ziwe na mwanga mkali sana na zitoshe kuwapa hofu tembo.

- Mbinu hii inaweza pia kutumika kufukuza viboko lakini kuwa makini kwani wanaweza wakakuvamia.

Weka uzio wa umeme

Mbinu hii ndiyo imebainika kuwa mbinu inayosaidia kwa muda mrefu. Ili kupunguza gharama za kuweka uzio wa aina hiyo unaweza kufanya mambo yafuatayo

- Uzio mmoja tu wa umeme uliowekwa mita 1.5 juu unatosha kabisa kuzuia tembo na wakati huo huo unaruhusu wanyama wadogo zaidi kupita chini yake.

- Tumia nguzo za mbao badala ya chuma ili kupunguza gharama.

- Tumia paneli za nishati ya jua kuizalisha umeme. Hata hivyo, huenda ukalazimika kutafuta mbinu za kulinda paneli hizo zisiibiwe.

Otesha mimea ambayo tembo hawapendi

Mashamba ya chaiPicha: DW/Cornelia Borrmann

Kama unaotesha mazao ya biashara, jaribu kuotesha yale ambayo tembo hawatayavamia. Ni kama vile tangawizi, cocoa, katani, chai, mimea izalishayo mafuta na hata pilipili.

Badilisha msimu wako wa kuotesha ama kuvuna

Kubadilisha kipindi cha kuotesha au kuvuna mara moja moja kunatosha kabisa kuwafukuza tembo.

Maajabu ya mnyama Tembo.

02:45

This browser does not support the video element.

Otesha mimea karibu na mimea mingine

Mimea inayooteshwa mbali na mimea mingine imeonekana kuwa katika hatari kubwa zaidi ya kuliwa na tembo kuliko mimea inayooteshwa karibu sana na mingine. Jaribu kuotesha mazao yako ama mboga mboga katika mashamba makubwa ya pamoja. Shirikiana na majirani zako kuotesha katika mashamba makubwa ya mraba na yaliyozungushiwa uzio wa miiba.

Piga kelele ama tengeneza kelele

Wakati mwingine, mlio wa risasi unaweza kufukuza kundi la tembo wanaovamia mashamba. Tatizo ni kwamba unatakiwa kuita wataalamu kufanya hivyo, kwahiyo unahitaji kuweka mipango mapema. Uliza mamlaka husika katika eneo unaloishi. Njia nyingine za kusababisha kelele ni hizi hapa:

- Watu kuita kwa sauti au kupiga mluzi kwa pamoja

- Kugonga vitu kama madebe, ngoma ama miti

- Kutegesha "alarm" kunaweza kusaidia kwa namna mbili: Kunaweza kukufahamisha kuwa kuna tembo na kunaweza pia kuwafukuza hao tembo kama sauti ya mlio huo ni kubwa sana.

Weka mizinga ya nyuki karibu na mazao yako

Picha: AFP/I. Ocon

Tembo wanaogopa nyuki. Ukiweka mizinga ya nyuki pembezoni mwa mashamba yako unaweza ukazuia tembo. Hata hivyo, utafiti kuhusu mbinu hii bado unafanyika.

Tembo wana tabia ya kunusa magamba ya miti kugundua kama tembo wengine walikojolea miti hiyo. Tembo anapokojolea miti anaonyesha kuwa anamiliki eneo fulani na kwa kawaida tembo wengine hawaendi tena kwenye eneo hilo. Unaweza kukusanya mkojo wa tembo kwenye bustani za kutunzia wanyama na kisha kuunyunyuzia kwenye mpaka wa mashamba yako.

Chanzo: wikiHow

Mwandishi: Elizabeth Shoo

Mhariri: Amina Abubakar