JKT Queens mabingwa wa Ngao ya Jamii
13 Oktoba 2025
Nchini Tanzania Jkt Queens wametawazwa kuwa Mabingwa wa Ngao ya Jamii kwa Wanawake Msimu wa 2025/26 baada ya kuwanyuka wapinzani wao wa jadi, Simba Queens Bao 2-1 katika fainali na kutwaa taji hilo kwa mara ya pili mfululizo.
Michuano ya Ngao ya Jamii, ilianza Kurindima rasmi mnamo Oktoba 9, ikiwashirikisha vigogo wanne wa soka la wanawake Yanga Princess,JKT Queens – mabingwa watetezi,Simba Queens na Mashujaa Queens.
Kocha wa Simba Queens Nsanganzelu Elieneza baada ya kuangukia pua Ubingwa wa Ngao ya Jamii anasema, ”Hakuna ambaye anapenda matokeo ya kupoteza sisi tulikuja kwa ajili ya kushinda na tulijiandaa kwa ajili ya kushinda Jkt wamefanya vizuri Zaidi na wameweza kupata hizo nafasi za kufanga kuna kitu tumejifunza Zaidi na tutaenda kukifanyia kazi uwanjani ili tuweze kurudi imara Zaidi”Amesema Kocha wa Simba Queens Nsanganzelu Elieneza
Kocha wa JKT Queens Kessy Juma anasema wao wameshavuka hatua za kushangilia Mataji badala yake wanataka kushangilia ubingwa wa Afrika.
"sisi hatuna furaha kwa sababu kama ni level hizi za kuchukua kombe hili Jkt Qeens wameshapita kwa hiyo sisi tunasubiri la Ligi ya Mabingwa ya wanawake Africa mechi ilikuwa ngumu mafanikio yetu ni kutokana na mchanganyiko wa nidhamu za kimbinu pamoja na kujituma kwa watoto wetu ushindi huu unatupa chachu ya kuendelea kupambana Zaidi ili kuiletea heshima Tanzania "Amesema Kocha wa JKT Queens Kessy Juma
Timu ya JKT Queens inaanza Maandalizi ya kujiandaa na Ligi ya Mabingwa ya Wanawake Afrika, iliyopangwa kufanyika nchini Algeria.
Taifa Stars yaendelea na maandalizi ya mashindano ya Kimataifa
Kando na Hayo macho na masikio ya Watanzania yanaelekezwa huko Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), ambako Timu ya Taifa ya Tanzania, itashuka dimbani kesho Oktoba 14, kucheza mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya timu ngumu ya Iran mchezo wa Kalenda ya FIFA.
Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya soka ya Tanzania ,Taifa Stars, Hemed Suleiman 'Morocco kuhusu Maandalizi ya mechi hiyo.
"Tupo vizuri kuhakikisha tunashinda hii mechi nafikiri itakuwa mechi ngumu na nzuri kwa sababu na sisi tumekua kwa kiasi Fulani ndio maana tunacheza mechi ya aina hii zamani tulikuwa hatupati nafasi za kucheza mechi za namna hii Timu ambayo inakua inacheza mechi kubwa za namna hii ni fursa kwetu kama Timu na ni fursa kwa vijana kuonesha kile ambacho wanancho na naamini itakuwa moja ya mechi nzuri”Amesema Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya soka ya Tanzania (Taifa Stars) Hemed Suleiman 'Morocco
Mchezaji wa Taifa Stars Bakari Mwamnyeto anasema wamejipanga vyema kukwaana na Iran.
"Sisi kama wachezaji tunajiandaa vizuri kuweza kuwakabili wapinzani wetu Iran kwa sababu ni Timu kubwa imetuzidi Ranks Tanzania lakini sisi sio wanyonge nadhani Iran wajipange vizuri wataona vipaji kutoka Tanzania na wategemee kuona mpira wenye ushindani kwa asilimia 100'Amesema Mchezaji wa Taifa Stars Bakari Mwamnyeto
Mechi hii ni sehemu ya maandalizi ya kikosi cha Stars kuelekea kampeni mbalimbali za kimataifa, ikiwemo AFCON.