Job Ndugai azikwa nyumbani kwake Kongwa, Tanzania
11 Agosti 2025
Safari ya mwisho ya maisha ya aliyekuwa Spika wa zamani wa bunge la Tanzania Job Yustino Ndugai leo imehitimishwa baada ya mwili wake kuhifadhiwa katika nyumba yake ya milele huko Shambani kwake katika kijiji cha Mandumbwa wilayani Kongwa mkoani Dodoma baada kufanyika ibaada ya mazishi iliyoongozwa na Askofu Mkuu wa kanisa la Anglikana Tanzania, Daktari Mahimbo Mndolwa kwenye kanisa la Mtakatifu Michael wilayani Kongwa.
Akizungumza katika ibaada ya mazishi ya marehemu Ndugai, Askofu Mndolwa amesema kuwa kuna baadhi ya watu waliopewa kipawa cha uongozi katika nafasi mbalimbali lakini wamekuwa wakitumia nafasi zao vibaya kwa kuwaumiza wengine na mewetaka watu wafuate mema aliyoyatenda spika wa zamani wa Bunge la Tanzania marehemu Job Yustino Ndugai.
“Unakifanyia nini kipawa alichokupa mungu. Wapo waliopewa kipawa cha mahela mengi, badala ya kujenga ufalme wa Mungu nan chi, wanakitumia kuumiza wengine. Wako waliopewa vipawa vya uongozi badala ya kuvitumia vizuri kuzalisha wengine, wanawafisha wengine. Tunapoelekea kuuzika mwili wa mtumishi huyu, Mungu akusaidie kupeleleza Mungu amekupa nini. Kama umepewa madaraka yatumie vizuri na usiyatumie vibaya.”
Majaliwa asema Ndugai alikuwa mwana mageuzi na mchapa kazi
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema marehemu Ndugai alikuwa mwana mageuzi na mmoja wa wanasiasa mashuhuri aliyebeba taswira ya wana Kongwa, mkoa wa Dodoma na kitaifa na kimataifa na kwamba serikali itayaenzi yale yote yaliyoasisiwa na marehemu Ndugai.
“Ndugu waombolezaji ni kwamba tunakumbuka jana mheshimiwa Rais wakati wa kuaga mwili wa mpendwa wetu pale Dodoma, pamoja na kutambua kazi kubwa na alama alizoacha marehemu ndani ya Kongwa kitaifa na kimataifa, aliagiza kukamilishwa masuala yote yaliyoanzishwa na marehemu, ikiwemo agizo kwa mamlaka husika kuendeleza kuitangaza Kongwa kama kielelezo cha makumbusho ya kupigania uhuru wa nchi za kusini mwa Afrika. Napenda kuwahakikishia wananchi wa Kongwa kuwa tutalisimamia agizo hili.”
Marehemu Job Ndugai alifariki dunia Agosti sita mwaka huu, wakati akipatiwa matibabu katika hospitali moja jijini Dodoma baada ya kuugua ghafla.
Wakati wa uhai wake alikuwa mbunge wa jimbo la Kongwa na aliwahi kuhudumu kama Spika wa Bunge la Tanzania tangu mwaka 2025 hadi alipojiuzulu nafasi hiyo mnamo mwaka 2022, hiyo ikiwa ni mara ya kwanza kwa Spika aliye madarakani kujiuzulu kwa hiyari yake katika historia ya Bunge la vyama vingi nchini Tanzania.