1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jobe Bellingham asajiliwa Borussia Dortmund

9 Juni 2025

Sunderland wamekubaliana na Borussia Dortmund ada ya uhamisho kumsajili kiungo Jobe Bellingham.

Familia ya Wachezaji wa Soka- Bellingham
Denise Bellingham (kushoto), Jude Bellingham (wa pili kushoto), Jobe Bellingham (wa pili kulia) na Mark Bellingham.Picha: David Davies/empics/picture alliance

 

Black Cats (jina la utani la Sunderland) wameafikiana ada ya rekodi ya klabu ya pauni milioni 33, pamoja na nyongeza ya pauni milioni 5 kama marupurupu kwa kinda huyo wa miaka 19, ambaye pia ni kaka mdogo wa kiungo wa timu ya taifa ya England, Jude Bellingham.

Ada hiyo itamfanya Jobe kuwa mchezaji wa pili kwa gharama kubwa zaidi kusajiliwa na klabu ya Bundesliga, nyuma ya Ousmane Dembele. Iwapo marupurupu hayo yatatimia, basi uhamisho huo utaweka rekodi mpya ya usajili kwa Dortmund.

Uhamisho huu pia ni mkubwa zaidi katika historia ya Sunderland, ukizidi ule wa Jordan Pickford kwenda Everton mwaka 2017.

Mkataba huo pia unajumuisha kipengele cha Sunderland kupata asilimia 15 ya mauzo ya baadaye ya mchezaji huyo. Hii ina maana kwamba Bellingham ataifuata njia aliyopitia kaka yake, ambaye alitumikia Dortmund kwa misimu mitatu kabla ya kutimiza ndoto yake ya kujiunga na Real Madrid majira ya kiangazi ya mwaka 2023.

Walipoanzia na muelekeo wao

Jude Bellingham kaka yake Jobe Bellingham akiitumikia timu ya Uhispania Real Madrid.Picha: Lluis Gene/AFP/Getty Images

Wote wawili, Jobe na Jude Bellingham, walianzia soka lao la kulipwa katika klabu ya Birmingham City, na Jobe aliamua kuhamia Sunderland majira ya kiangazi miaka miwili iliyopita.

Katika kipindi cha miaka miwili, alicheza michezo 90, akifunga mabao 11 na kutoa asisti nne. Alikuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya Sunderland kwenye ligi ya Championship msimu uliopita, lakini kipaji chake kilikuwa kikifuatiliwa kwa karibu na vilabu kadhaa — ikiwa ni pamoja na Eintracht Frankfurt, pamoja na RB Leipzig.

Hata hivyo, kuondoka kwake kulionekana kuwa hakuepukiki kadri muda ulivyoenda. Licha ya hayo, Sunderland walikuwa na msimamo wa kutomuacha aondoke kwa bei ya chini ya thamani waliyoipanga, na bei ya mwisho imeongezeka sana kutoka ofa ya awali ya Dortmund, ambayo inaeleweka kuwa ilikuwa karibu pauni milioni 20.

Katika Borussia Dortmund, Bellingham anatarajiwa kujiunga na timu ya kwanza na kushiriki katika michuano ya Kombe la Klabu la Dunia, linalotarajiwa kuanza Juni 17, ambapo Dortmund itakutana na timu kama Fluminense, Mamelodi Sundowns, na Ulsan Hyundai. Hatua hii inamuweka Jobe Bellingham katika njia ya kufuata nyayo za kaka yake Jude, alieshiriki katika Bundesliga akiichezea Dortmund na vile vile kuimarika kimchezo kabla ya kuhamia Uhispania.

Kwa upande mwingine, Sunderland imejizatiti kumuuza winga Tommy Watson kwa Brighton kwa pauni milioni 10 na kufanya uhamisho wa kudumu wa Enzo Le Fée kutoka Roma kwa pauni milioni 20. Kocha wa Sunderland, Régis Le Bris, amemsifu Bellingham kama mchezaji mwenye ushindani mkubwa na uwezo wa kipekee.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW