1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Joe Biden aonekana kung'ara licha ya misukosuko

Deo Kaji Makomba
4 Machi 2020

Katika kipindi cha chini ya mwezi mmoja uliopita, kampeni za mgombea wa chama cha Democratic Joe Biden zilikuwa katika hatari ya kusambaratika.

Mgombea wa chama cha Democratic Joe Biden
Mgombea wa chama cha Democratic Joe BidenPicha: picture-alliance/dpa/AP/G. Broome

Katika kipindi cha chini ya mwezi mmoja uliopita, kampeni za mgombea wa chama cha Democratic Joe Biden zilikuwa katika hatari ya kusambaratika. Na hata baada ya kurejea kwa kishindo kikubwa kufuatia ushindi kwenye jimbo la South Carolina, alijikuta akikabiliana na uhalisia wa kushindana kwenye mpambano muhimu wa Jumanne Maalumu ama Super Tuesday, akiwa na fedha kidogo lakini pia kampeni yake haikuwa na miondombinu imara.

Makamo huyo wa Rais wa zamani wa Marekani, alipata ushindi mkubwa kwenye chaguzi za awali za chama cha Deomocratic kwenye majimbo mengi nchini humo. Ameungwa mkono na matabaka mengi ya watu, kuanzia  wapiga kura weusi, wanawake, wazee na wasomi wa vyuo mbalimbali ambao wote walivutiwa na kampeni zake. Mgombea ambaye awali alionekana kama anayeporomoka, Biden hivi sasa ndiye anayeonekana kupigiwa upatu zaidi na chama chake cha Democratic.

Majimbo muhimu yampigia kura Biden 

Jimbo la California, lilikuwa ni miongoni mwa mwa majimbo machache ambayo Biden ameyapoteza kwa seneta wa jimbo la Vermont, Bernie Sanders. Lakini Biden alichukua Texas ambalo ni jimbo la pili kwa ukubwa pamoja na majimbo mengine manane. Ushindi wake katika majimbo ya Virginia na North Carolina ambayo ni majimbo mawili yenye umuhimu mkubwa kwenye maamuzi katika uchaguzi mkuu wa majimbo, ulikuwa na umuhimu wa kipekee.

Nguvu mpya aliyoipata Biden inamuweka  ana kwa ana na mgombea mwingine Bernie Sanders na ambapo chama chao kitaamua nani atakayeweza kupeperusha bendera kuiwakilisha Democratic mnamo mwezi Novemba.

Mpinzani wa Joe Biden, Bernie Sanders kwa ticketi ya chama cha DemocraticPicha: Reuters/J. Ernst

Mliberali Sanders, kwa muda mrefu amekuwa akitoa mwito wa mabadiliko makubwa kwenye sekta ya huduma za afya na uchumi, huku Biden ambaye ana misimamo ya wastani na kampeni zake ambazo hazikujikita kwenye itikadi, zaidi anaonekana kama mgombea anayetarajia kubadilisha mweleko wa taifa hilo ikiwa atafanikiwa kumng'oa mamlakani Rais Donald Trump.

Changamoto kwa Trump?

Wengi kwenye chama cha Democrat walitambua kwamba Sanders alikuwa akinufaika zaidi na makundi ya wagombea wenye misimamo ya wastani ambao walikuwa wanazigawa kura za chama hicho. Lakini haikuwa hivyo hadi pale Biden alipopata ushindi mkubwa katika jimbo la South Carolina siku ya Jumamosi na ndipo walipoanza kumuona kama mbadala bora zaidi.

Mgombea mwingine aliyekuwa akipigiwa upatu, Seneta Elizabeth Warren alishindwa kutamba hata kwenye jimbo la nyumbani kwake la Massachusetts alipoibuka katika nafasi ya tatu. Ni kutokana na hilo sasa, chama cha Democratic kinasalia na wagombea wawili weupe Bernie na Sanders ambao wote wakiwa na umri wa zaidi ya miaka ya 70, kupambana kupeperusha bendera ya chama hicho kinachokabiliwa na mgawanyiko.

Mbio hizi zinafanana na zile za mwaka 2016 dhidi ya mgombea wa wakati huo, Hillary Clinton, ambaye alikuwa na misimamo ya wastani zaidi na aliyeonekana kama chaguo bora zaidi hadi pale Donald Trump alipoibuka na ushindi wa kushangaza katika uchaguzi mkuu. Sanders na wafuasi wenzake wanaomba chama hicho kutochukua mkondo kama huo kwenye uchaguzi wa safari hii.

Ni hakika kwamba Biden anasalia kama mgombea anayekabiliwa na hatari. Amekosa mvuto kwa wapiga kura vijana huku akitofautia na kundi la la mrengo wa kushoto lenye hamasa kubwa ndani ya chama hicho.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW