Johannesburg: Mbeki azungumza kwa simu na Mugabe.
25 Machi 2007Rais Thabo Mbeki wa Afrika kusini amekua na mazungumzo ya simu na rais wa Zimbabwe Robert Mugabe, kufuatia kupamba moto kwa kampeni dhidi ya wafuasi wa upinzani nchini Zimbabwe. Gazeti la The Sunday Times nchini Afrika kusini lilimnukulu afisa mmoja wa ngazi ya juu mjini Johannesburg akikiri kwamba Rais Mbeki ambaye amekua akikosolewa kwa kukaa kimya kuhusu mgogoro wa kisiasa na kiuchumi nchini Zimbabwe amezungumza na Mugabe , lakini akakataa kueleza kilichozungumzwa. Jana Rais Mugabe mwenye umri wa miaka 83 aliwataka wafuasi wake kujiandaa kwa uchaguzi wa rais na bunge mwaka ujao, matamshi ambayo yanaashiria huenda amesalimua amri kufuatia shinikizo ndani ya chama chake atawala ZANU-PF kupinga mpango wa kutaka kurefusha muda wa utawala wake hadi 2010. Mugabe anaitawala Zimbabwe kwa miaka 27 sasa ikiwa ni tangu uhuru 1980.