1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

John Bolton, Afghanistan na bajeti ya Ujerumani Magazetini

Oumilkheir Hamidou
11 Septemba 2019

Mshauri wa rais wa Marekani Donald Trump wa masuala ya usalama wa taifa, John Bolton atimuliwa ikulu ya Marekani, hali nchini Afghanistan na bajeti ya serikali kuu ya Ujerumani ni miongoni mwa mada magazetini.

Bundestag | Haushaltsdebatte | Finanzminister Olaf Scholz
Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Tunaanzia Marekani ambako rais Donald Trump ametangaza kumfukuza kazi mshauri wake mashuhuri na muhimu wa masuala ya usalama wa taifa John Bolton. Habari za kufukuzwa kwake ikulu ya white House zimepokelewa kwa hisia tofauti na wahariri wa magazeti ya Ujerumani.

Mhariri wa gazeti la "Allgemeine Zeitung" anaandika :"Kwa vyovyote vile, kufukuzwa ikulu ya Marekani John Bolton kumeifanya dunia iwe salama japo kidogo. Bila ya shaka tusidanganyike na kufikiri hivi sasa rais Donald  Trump ni wa kuaminika. Hata hivyo dalili zinaongezeka na kuonyesha kwambaTrump hachelei kitu anapodhamiria kulifikia lengo lake. Na ikiwa hana njia nyengine, hachelei pia kubadailisha msimamo wake, akihakikisha watakaolaumiwa ni wengine."

 Hali ya kuhuzunisha Afghanistan

"Hatima ya Afghanistan haijulikani.Mazungumzo ya amani kati ya Marekani na wanamgambo wa itikadi kali wa Taliban yamevunjika na damu inazidi kumwagika nchini humo. Gazeti la "Hannoversche Allgemeine" linaandika:"Ni mkosi mkubwa na wa kuhuzunisha. Shughuli za tume ya kimataifa ya kulinda amani nchini Afghanistan zinaingia mwaka wake wa 19 na hakuna dalili ya kupatikana ufumbuzi wa mzozo wa nchi hiyo. Kinyume kabisa: Habari za kuhuzunisha ndizo zinazosikika kutoka Afghanistan.

"Mashambulio dhidi ya watu wanaosherehekea harusi, mashambulio dhidi ya mashirika ya kimataifa, na shambuluo jengine la bomu limeripuka ndani ya gari siku chache baadae. Dazeni wamekufa katika mashambulio hayo  mnamo wiki zilizopita. Idadi ya mashambulio dhidi ya shule imeongezeka kupita kiasi mwaka 2018. Shule zaidi ya 100 zimelazimika kufungwa. Wafuasi wa itikadi kali wa Taliban wanaonyesha wanasonga mbele."

Bajeti ya serikali kuu haina nakisi

Mada yetu ya tatu magazetini inaturejesha hapa hapa Ujerumani ambako waziri wa fedha  wa serikali kuu Olaf Scholz ametangaza bajeti mpya ya shirikisho. Maoni ya wahariri yanatofautiana pia kuhusiana na suala kama serikali kuu italazimika kukopa au la ili kukidhi mahitaji yote muhimu. Gazeti la Reutlinger General-Anzeiger linaandika:"Kila mmoja  anazungumzia kuhusu bajeti bila ya nakisi, ila Olaf Scholz. Lakini si siri kwa yeyote kwamba waziri wa fedha anaiogopa kupita kiasi fikra ya kuchukua mkopo. Hataki asaije akawapa watu sababu ya kusema eti kwasababu ni waziri wa fedha kutoka chama cha SPD ambacho ni cha rangi nyekundu, ndio maana bajeti yake imepindukia mstari mwekundu.

Olaf Scholz anatajwa kuwaa mwanasiasa imara na hivyo hivyo ndivyo bajeti yake inavyobidi iwe. Bajeti bila ya nakisi ndio aliyoirithi kutoka kwa mtangulizi wake, Wolfgang Schäuble wa chama cha CDU. Anaweza kuashiria makelele yatakuwa ya aina gani akipindukia.

Ukweli lakini ni kwamba bajeti ya waziri wa fedha inazongwa na vipenmgee visisvyokuwa na idadi. Serikali ikipitisha mpango wake kuhusu mabadiliko ya tabianchi septemba 20 inayokuja, basi Olaf Scholz atalazimika kutumia ustadi wake kama mshika hazina ili kuepusha balaa la nakisi ya bajeti.

 

Chanzo: Magazeti ya Ujerumani