John Kerry awasili Sudan Kusini
2 Mei 2014Ziara hiyo ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani inaonekana kuwa ni hatua mojawapo ya kumaliza mapigano yanayoendelea kati ya wanajeshi wa serikali ya Sudan Kusini inayoongozwa na Salva Kiir pamoja na waasi wanaoongozwa na aliyekuwa makamu wa rais wa nchi hiyo, Riek Machar.
Kerry atakutana na rais wa nchi hiyo Salva Kiir ili kujadiliana naye kuhusu jinsi ya kuvikomesha vita hivyo vilivyodumu kwa kipindi cha miezi minne sasa.
"Waziri Kerry atasisitiza umuhimu wa pande zote kuheshimu makubaliano ya kuacha uadui, kusitisha mara moja kuwashambulia raia pamoja na kushirikiana kikamilifu na Umoja wa Mataifa pamoja na mashirika ya kibinaadamu" amesema msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani, Jen Psaki.
Kerry pia anatazamiwa kukutana na viongozi wa jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa ambalo limekuwa likishambuliwa na pande zinazoendelea na mapigano wakati likiwa linapambana kukabiliana na uovu unaoendelea.
Hali kadhalika Kerry atakutana na viongozi wa asasi za kiraia pamoja na machifu wa jumuiya mbalimbali wa nchi hiyo.
Wito wa kusimamisha mapigano
Kerry amewasili Juba akitokea Addis Ababa, Ethiopia. Akiwa Ethiopia hapo jana, Kerry alitoa onyo kwa pande zinazopigana Sudan Kusini kusitisha vita hivyo.
"Haya bila shaka ni machafuko ambayo umma wa Sudan Kusini ulipigana kwa nguvu na kwa muda mrefu kuyaepuka na Marekani na nchi nyingine zikahusika vilivyo kujaribu kulifanya hilo litokee kwa mkataba wa amani, kura ya maoni na hatimaye uhuru wa taifa hilo". Amesema.
Marekani ilisaidia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa uhuru wa taifa la Sudan Kusini mwaka 2011 na ziara hiyo ya Kerry inachukuliwa kama kiashiria cha kuongezeka mashaka kwa Marekani ya jinsi gani taifa hilo changa limeingia katika machafuko katika kipindi kifupi toka lipate uhuru.
Kutokana na machafuko hayo, maelfu ya watu wameshauwawa huku karibu watu millioni moja wamekimbia makazi yao wengi wao wakiwa wamepata hifadhi katika kambi za Umoja wa Mataifa ili kuepusha kuuwawa.
Mwandishi: Anuary Mkama/AFPE/RTRE
Mhariri: Josephat Charo