1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaGhana

Ghana : Mahama apata ushindi wa kihistoria katika uchaguzi

Saleh Mwanamilongo
9 Desemba 2024

Rais wa zamani wa Ghana John Drahami Mahama ashinda uchaguzi na tayari mgombea wa chama tawala amekiri kushindwa hata kabla ya matokeo rasmi kutangazwa na tume ya uchaguzi.

Rais mteule wa Ghana John Drahami Mahama
Rais mteule wa Ghana John Drahami MahamaPicha: Misper Apawu/AP/picture alliance

Tume ya uchaguzi ya Ghana bado haijatoa matokeo rasmi, lakini Mahamudu Bawumia, makamu wa Rais na mgombea wa chama tawala cha New Patriotic, alikiri kushindwa. Bawumia alitangaza kuwa Waghana walitaka mabadiliko.

"Mabibi na mabwana, tumekubali kushindwa kama mwanademokrasia mkamilifu angefanya. Lakini hatujaachana na vita vya kubadilisha Ghana na kupanua fursa kwa makundi yote ya jamii yetu. Hatutakuwa upinzani wa kuvuruga.", 

Kushindwa kwake kumemaliza miaka minane madarakani kwa chama cha NPP chini ya Rais Nana Akufo-Addo, ambaye muhula wake wa mwisho ulikumbwa na msukosuko mbaya zaidi wa kiuchumi katika taifa hilo la Afrika Magharibi. Kwa miaka mingi, Ghana ilishuhudia mfumuko mkubwa wa bei na kushindwa kulipa madeni.

Mgombea wa chama cha upinzani cha National Democratic Congress, John Drahami Mahama, ametarajiwa kutangazwa mshindi na tume ya uchaguzi. Mahama aliwahi kuwa rais wa Ghana kutoka 2012 hadi 2017. Na hili lilikuwa jaribio lake la tatu kugombea tena urais baada ya kushindwa katika chaguzi za 2016 na 2020.

Matokeo rasmi kutangazwa Jumanne

Tume ya uchaguzi imesema huenda matokeo rasmi yakatangazwa kufikia siku ya JumannePicha: Julius Mortsi/ZUMAPRESS/picture alliance

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Jean Mensa baadaye Jumapili alihimiza uvumilivu, baada ya mvutano kati ya vyama katika baadhi ya vituo ya kupigia kura kufuatia kucheleweshwa kutangaza matokeo.

Hata hivyo vyama vya kisiasa vilikuwa na mawakala wao katika vituo vya kupigia kura, ambao walichunguza na kujumlisha matokeo ya awali.

Mahama bado hajazungumza hadharani. Lakini kwenye akaunti yake ya X, alithibitisha kupokea simu ya pongezi kutoka kwa mgombea wa chama tawala kutokana na "ushindi wake mkubwa".

Ubalozi wa Marekani mjini Accra pia ulipongeza huo ukiuita kuwa wenye mafanikio na unaoakisi mapenzi ya watu wa Ghana. Marekani imeahidi kuendeleza ushirikiano wake wenye nguvu chini ya utawala wa rais mpya.

Uchumi mada kuu ya kampeni

Matatizo ya kiuchumi na mfumuko wa bei vilighubika kampeni za uchaguzi, baada ya nchi hiyo,  ya kwanza kutika uzalishaji dhahabu barani Afrika na mshafirishaji wa pili wa kakao duniani, kupitia mgogoro wa kushindwa kulipa madeni na kuporomoka kwa thamani ya fedha, na kusababisha mkopo wa dola bilioni 3 kutoka kwa Shirika la Fedha Ulimwenguni, IMF. Hata hivyo, uchaguzi huo tulivu na wa amani umeonyesha ukomavu wa demokrasia nchini Ghana.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW