1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Johnson alazwa chumba cha wagonjwa mahututi

7 Aprili 2020

Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson amepelekwa tangu Jumatatu usiku katika chumba cha wagonjwa mahututi na majukumu yake amempa waziri wa mambo ya nje Dominic Raab

England | Coronavirus | Britischer Premierminister Johnson auf Intensivstation
Picha: AFP/T. Akmen

Nchini Uingereza waziri mkuu Boris Johnson amelazwa tangu jumatatu usiku kwenye chumba cha wagonjwa mahututi baada ya hali yake kuzidi kuwa mbaya na kuzusha wasiwasi hii leo kuhusu hatma ya afya yake na jinsi serikali inavyoushughulikia mripuko huu wa virusi vya Corona unaozidi kuonekana ukisambaa nchini humo.

Waziri mkuu huyo amemtaka waziri wake wa mambo ya nje Dominic Raab kuchukua majukumu ya uongozi muda mfupi kabla hajapelekwa chumba cha wagonjwa mahututi  katika hospitali ya St Thomas mjini London.

Picha: AFP/10 Downing Street

Kimsingi Boris Johnson alifikishwa hospitali jumapili ikiwa ni siku 10 baada ya kugundulika ameambukizwa virusi vya Corona wakati huo bado alikuwa na dalili za kukohoa sana na joto kali la mwili. Boris Johnson ana umri wa miaka 55 na kupelekwa kwake kwenye chumba cha wagonjwa mahututi kumezusha wasiwasi lakini ujumbe wa kumtakia ahueni umemiminika kotoka matabaka mbali mbali ya watu nchini Uingereza na duniani kwa Jumla.

Huko Japan waziri mkuu Shinzo Abe ameamua kuongeza tahadhari kwa kutangaza hali ya dharura ya kupambana na kusambaa kwa virusi hivyo. Hali hiyo ya dharura ya kiasi mwezi mmoja imetangazwa kwa mji wa Tokyo na miji mingine sita yenye asilia 44 ya idadi ya watu nchini humo.

Picha: Imago Images/Aflo

Waziri mkuu Abe pia ametangaza mbele ya bunge mpango wa kusaidia uchumi wa dolla bilioni 990 kukabiliana na athari zitakazosababishwa na virusi vya Corona katika nchi hiyo ya tatu kiuchumi duniani.Kwa upande mwingine hapa nchini Ujerumani taasisi ya kufuatilia na kudhibiti magonjwa ya kuambukiza ya Robert Koch imesema leo kwamba ni mapema mno kuzungumzia juu ya kupungua kwa visa vipya vya maambukizi nchini Ujerumani.

Rais wa taasisi hiyo Lothar Wieler amesema Ujerumani inabidi isubiri siku chache kutazama mwelekeo wa hali inavyokwenda.Kadhalika taasisi hiyo ilibaini kwamba maambukizi ya virusi hivyo yameongezeka kwa idadi ya 3,834 katika kipindi cha saa 24 na kuifanya idadi ya walioambukizwa kufikia leo Jumanne nchini Ujerumani kufikia 99,225,ikiwa ni idadi iliyoongezeka baada ya siku nne ya kuonekana matumaini ya kuteremka kwa maambukizi.

Na China hakuna vifo vipya vilivyoripotiwa siku moja baada ya kuondowa vizuizi vya usafiri kutoka mji wa Wuhan ambako ni kitovu cha mripuko wa virusi vya Corona. Hata hivyo kuna mashaka kwamba Beijing inaendelea kwa makusudi kutowa taarifa zisizosahihi kuhusu idadi halisi ya vifo na maambukizi nchini humo,ingawa China inayapinga madai hayo. Katika eneo la ghuba,wito umetolewa na shirika la haki za binadamu Human Rights Watch wa kuizitaka nchi za eneo hilo kuwaachia huru wanaharakati wa kisiasa wanaoshikiliwa jela na kupunguzwa pia idadi ya wafanyakazi wakigeni wanaozuiliwa ili kupunguza hali ya kusambaa kwa virusi hivyo vya Corona.

Picha: Reuters/C. Pike

Human Rights Watch imezitaja Bahrain Kuwait,Oman,Qatar,Saudi Arabia na Umoja wa GFalme za kiarabu kwamba zinawashikilia maelfu ya wafanyakazi wakigeni kwa madai ya kukiuka sheria za ukaazi.Na kwa upande wa Afrika hivi sasa kuna zaidi ya visa 10,000 vya maambukizi ya virusi hivyo kwa mujibu wa vituo vya kudhibiti na kuzuia magonjwa vya barani humo. Nchi 52 kati ya 54 za bara hilo kufikia leo Jumanne zimetajwa kuwa na maambukizi,Sao Tome na Principe ikiwa nchi ya karibissa kuripoti maambukizi huko visiwa vya Comoro na Lesotho zikiwa nchi pekee za bara hilo ambako hakuna mgonjwa wa COVID-19.

Mwandishi:Saumu Msimba

Mhariri-Josephat Charo

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW