1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Johnson kitanzini baada ya mawaziri zaidi kuachia ngazi

Sylvia Mwehozi
6 Julai 2022

Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson ameendelea kukabiliwa na shinikizo la serikali yake baada ya mawaziri wengine wawili kuachia ngazi baada ya mawaziri wa afya na fedha nao kujiuzulu kutokana na madai ya kashfa.

Großbritannien Premierminister Boris Johnson
Picha: Matt Dunham/AP Photo/picture alliance

Waziri wa watoto na familia Will Quince ametangaza kujiuzulu nafasi yake hii leo wakati waziri mdogo wa usafirishaji Laura Trott naye akibwaga manyanga kwa madai ya kukosa "imani" na serikali. Mbunge mdogo Robin Walker katika serikali ya Jonhson, naye amejiuzulu kama waziri wa masuala ya shule hii leo, ikiwa ni hatua ya hivi karibuni katika wimbi la mawaziri kujiuzulu kuhusiana na uongozi wa Johnson.

Jumanne jioni, waziri wa fedha Rishi Sunak na mwenzake wa afya Sajid Javid walitangaza kujiuzuluwakidai kwamba hawawezi kuendelea kuvumilia kashfa ambazo zimemkabili Johnson kwa miezi kadhaa. Sasa watarejea viti vya nyuma vya chama cha Conservative bungeni wakati wa mkutano wa kila wiki wa maswali kwa waziri mkuu bungeni, wakiapa kuwa wakali kuliko hapo awali.

Kujiuzulu kwa Sunak na Javid, kulitangazwa dakika chache baada ya waziri mkuu Johnson kuomba radhi kwa kumteua afisa mwandamizi wa chama cha Conservative ambaye wiki iliyopita alijuzulu baada ya kushutumiwa kwa kuwapapasa wanaume wawili kwa ulevi. Waziri wa zamani wa elimu Nadhim Zahawi ndiye ameteuliwa kuwa waziri wa fedha.

Waziri mpya wa fedha wa Uingereza Nadhim Zahawi Picha: Avalon/Photoshot/picture alliance

Waziri huyo mpya wa uchumi tayari ameahidi kushughulikia uchumi ambao umeyumba akiongeza kwamba atazingatia njia zote za kukuza uchumi ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kupunguzwa kwa kodi. Uchumi wa Uingereza unaonyesha dalili za wazi za kudorora wakati mfumuko wa bei ukielekea katika tarakimu mbili na kutabiriwa kuwa dhaifu kuliko mataifa mengine makubwa yenye uchumi wa kiviwanda mwaka ujao.

Zahawi, anayejulikana sana katika chama cha Conservative kwa usimamizi thabiti wa utoaji chanjo ya COVID-19 nchini Uingereza, alisema kuwa mwaka 2023 unatarajiwa kuwa "mgumu sana" na atajielekeza katika suala la kupanda kwa gharama za maisha zinazokabili kaya nyingi.

"Nitatizama kila kitu, hakuna nitakachoacha. Waziri mkuu anataka kuhakikisha kwamba tuna nidhamu ya fedha. Tukishindwa kudhibiti mfumuko wa bei itakuwa ni uharibifu mkubwa kwa watu wale wale ambao tunajaribu kuwasaidia leo. Lakini, bila shaka, nitakuwa nikiangalia ni wapi pengine ninaweza kuhakikisha kwamba uchumi unabaki kuwa wa ushindani na wenye nguvu, unajua, majirani zetu wa Ulaya na bila shaka dunia nzima pia", alisema waziri mpya wa fedha.

Waziri Mkuu Johnson amekabiliwa na kashfa mbalimbali ikiwemo ile ya "Partygate"na kujikuta akipigwa faini ya polisi kwa kuvunja vizuizi vya kukabiliana na janga la Covid-19. Waziri Mkuu huyo mwenye umri wa miaka 58 bado anakabiliwa na uchunguzi wa bunge wa iwapo aliwadanganya wabunge kuhusu ukiukwaji wa vizuizi wakati wa sherehe katika mtaa wa Downing.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW