Jordan, Ujerumani zataja jukumu la UN kikosi cha Gaza
1 Novemba 2025
Jordan na Ujerumani zimesema hii leo kwamba kikosi cha kimataifa kinachotarajiwa kusaidia polisi wa Palestina huko Gaza, chini ya mpango wa Rais Donald Trump wa baada ya vita, lazima kiwe na mamlaka ya Umoja wa Mataifa.
Waziri wa mambo ya nje wa Jordan Ayman Safadi amesema ili kikosi hicho kiweze kuwa na ufanisi, ni lazima kipate mamlaka kutoka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Safadi alikuwa akizungumza katika kongamano la mjini Manama nchini Bahrain, pamoja na mwenzake wa Ujerumani Johann Wadephul, ambaye pia ameunga mkono jukumu la Umoja wa Mataifa kwa kikosi hicho akisema kitahitaji msingi wa wazi katika sheria za kimataifa.
Kikosi hicho kinachojulikana kama kikosi cha kimataifa cha kuleta utulivu, kinatakiwa kutoa mafunzo na kuwasaidia polisi wa Palestina walioidhinishwa na kuungwa mkono na Misri na Jordan.