1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jordan yachagua baraza la wawakilishi

Elizabeth Shoo23 Januari 2013

Uchaguzi huo umesusiwa na makundi ya watu wenye msimamo mkali wa Kiislamu. Wagombea 1,400 wanawania viti 150 . Mfalme Abdullah wa pili ndiye mwenye madaraka makubwa zaidi kuliko wanasiasa watakaochaguliwa.

Mabango ya uchaguzi jordan
Mabango ya uchaguzi jordanPicha: DW/ Mohamad AL Anasweh

Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa saa moja asubuhi kwa saa za Jordan na vitafungwa leo saa moja jioni.  Watu wapatao milioni 2.2 wamejiandikisha kupiga kura lakini saa tatu baada ya vituo kufunguliwa, tume ya uchaguzi iliripoti kwamba ni watu 125,000 tu waliofika kupiga kura.  Idadi hiyo ndogo kwa sehemu inatokana na uamuzi wa chama cha Udugu wa Kiislamu, ambacho ni chama kikubwa zaidi cha upinzani, kususia uchaguzi.  Makamu mwenyekiti wa chama hicho, Zaki Bani Rsheid, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba hatarajii kuwa bunge litakalochaguliwa litadumu kwa muda mrefu kwani halitakuwa na nguvu ya kisiasa.

Taufiq Abu Ischir ni mhandisi aliyesomea hapa Ujerumani.  Yeye hana matarajio makubwa na uchaguzi wa leo. "Wanaharakati wengi, walioandamana kudai mabadiliko ya sera, wamesusia uchaguzi.  Inamaana kwamba sura zile zile zitarejea bungeni.  Inasemekana kuwa bunge litapewa madaraka zaidi, na mfalme kupunguziwa madaraka, lakini nadhani kwamba mambo yatabakia kama zamani."

Raia wanataka mabadiliko

Ni jambo linalofahamika wazi kwamba wabunge wengi wana uhusiano wa karibu na Mfalme Abdullah wa pili.  Vyama vya upinzani vilitaka wananchi wenyewe wapewe nafasi ya kumchagua waziri mkuu lakini jambo hilo halikukubaliwa na Mfalme.  Hata hivyo ametoa mamlaka hayo kwa bunge ambalo hata sasa lina uwezo wa kuwachagua mawaziri.  Hapo awali, mawaziri na waziri mkuu walichaguliwa moja kwa moja na Mfalme.

Ali Mansour ni raia wa Jordan. Hata yeye hana matumaini kwamba patakuwa na maendeleo yoyote baada ya uchaguzi. Yeye ni mmoja wa wale waliosusia uchaguzi. “Mimi siiamini hii ndoto ya kwamba mfumo wa kisiasa utabadilika," anasema Mansour. "Tunatakiwa kwanza kuunda misingi ya kidemokrasia ili kila mgombea mwenye nia njema ya kisiasa aweze kuwa na nafasi sawa na wagombea wengine. Hilo likitimia ninaweza kufikiria juu ya kupiga kura."

Polisi wa Jordan wakitoa ulinzi wakati wa maandamano ya wafuasi wa chama cha Udugu wa KiislamuPicha: Reuters

Matatizo bado ni mengi

Jordan inakumbwa na matatizo mbali mbali ikiwemo nakisi ya bajeti inayofikia dola za kimarekani bilioni 5. Ukosefu wa ajira nao ni tatizo kwani idadi kubwa ya vijana hawana nafasi za kazi. Takwimu rasmi zinaeleza kwamba asilimia 14 ya wananchi wa Jordan hawana ajira lakini taasisi zisizo za serikali zinaarifu kuwa kiwango hicho kinafikia asilimia 30.

Matokeo ya uchaguzi yanatarajiwa kuanza kutolewa saa mbili baada ya vituo vya kupigia kura kufungwa. Matokeo rasmi yamepangwa kutolewa kesho.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/afp/dpa

Mhariri: Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi