1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSyria

Jordan yashutumiwa kufanya shambulio la anga Syria

Hawa Bihoga
31 Agosti 2023

Shambulio la anga la mapema Alhamisi dhidi ya kinachodaiwa kuwa kiwanda cha dawa za kulevya kusini mwa Syria karibu na mpaka na Jordan, limesababisha uharibifu, inagawa hakujatolewa taarifa kuhusu vifo.

Syrien Damaskus Explosionen im Osten der Stadt
Picha: Muhammad Khair/AA/abaca/picture alliance

Wanaharakati wa upinzani Syria wamesema, inaaminika shambulio hilo limetekelezwa na wanajeshi wa kikosi cha anga cha Jordan.

Vyombo vya habari vya serikali ya Jordan viliripoti wiki kadhaa zilizopita kwamba ndege kadhaa zisizo na rubani zilizokuwa na mihadarati zilidunguliwa baada ya kuvuka kutoka Syria.

Kiwanda cha Captagon kimekuwa kikishukiwa na Jordan, kadhalika Saudi Arabia na mataifa mengine ya Ghuba, kwani mamilioni ya vidonge yamekuwa yakisafirishwa kwa miaka mingi.

Soma pia:Miripuko yailenga ghala la maroketi nchini Syria

Dawa hizo hutumiwa kwa burudani na watu walio na kazi ngumu ili kuwafanya wasilale.

Ahmad al-Masalmeh, mwanaharakati wa upinzani ambaye anafuatilia matukio ya kusini mwa Syria alisema eneo hilo pia lilitumika kama ghala la kuhifadhia mihadarati.

Alisema wasafirishaji wa dawa za magendo huziandaa dawa hizo haramu ikiwemo kuzifungasha kabla ya kuzisafirisha kuvuka mpaka wa kusini hadi Jordan.

Mashirika ya kiutu Syria yathibitiha shambulio hilo

Shirika la ufuatiliaji wa masuala ya haki za binadamu na vita nchini Syria lenye makao yake makuu nchini Uingereza limeripoti juu ya shambulio hilo na kusema kiwanda kimeharibiwa.

Moshi ukiwa angani baada ya shambulioPicha: Baderkhan Ahmad/AP/picture alliance

Wakati huo huo kituo cha radio nchini humo kinachounga mkono serikali cha Sham FM, kimeripoti pia na kusema shambulio hilo, limepiga pia kwenye shamba na kusababisha uharibifu wa mazao, lakini hakikusema kuhusiana na vifo wala majeruhi.

Soma pia:Iran: Mashambulizi dhidi ya Syria huenda yakachochea visasi

Shambulio hilo limetokea kwenye kijiji cha Um Rumman, hatua chache na mpaka na Jordan, katika jimbo la Sweida eneo ambalo maandamano dhidi ya serikali yameendelea kwa wiki ya pili.

Mwezi Mei, shambulio la anga dhidi ya kijiji katika jimbo la kusini la Sweida lilimuua kigogo maarufu wa dawa za kulevya wa Syria na familia yake, ambapo wanaharakati wanaamini kwamba lilifanywa na Jordan.

Jordan haijajibu shutuma za shambulio

Jordan haijawahi kuthibitisha wala kukanusha kufanya shambulio la anga la mwezi Mai, lakini imesema mara kadhaa kwamba itatumia nguvu katika kupambana na magendo kuvuka mpaka. 

Si maafisa wa Jordan au vyombo vya habari vya nchini humo vilivyotoa kauli juu ya shambulio la Alhamisi.

Shambulio hilo limefanyika wakati Jordan, Saudi Arabia na nchi nyingine za Kiarabu zikiendelea kufanya kazi ya kusawazisha uhusiano na Damascus, baada ya kuitenga Syria kutokana na ukandamizaji wa kikatili wa Rais Bashar Assad dhidi ya waandamanaji mwaka 2011.

Rais Assad uso kwa uso na viongozi mataifa ya Kiarabu

00:54

This browser does not support the video element.

Machafuko hayo yaligeuka vita vya wenyewe kwa wenyewe, ambavyo sasa vimeingia mwaka wake wa 13, vikiligawa taifa na kuuwa raia zaidi ya 300,000, katika muongo mmoja, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Soma pia:Miaka 10 baada ya shambulizi la kemikali Ghouta nchini Syria

Marekani, Uingereza pamoja na serikali za nchi za Magharibi zimemshutumu Assad na washirika wake katika serikali ya Syria yenye uhaba wa fedha kwa kuongoza katika uzalishaji wa dawa aina ya Captagon.

Miongoni mwa hatua walizochukua ni pamoja na kuwawekea vikwazo jamaa wa Assad, wafanyabiashara na washirika wengine nchini Syria kwa kuhusika kwao katika sekta hiyo.


 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW