1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jose Manuel Barroso azomewa Lampedusa

Admin.WagnerD9 Oktoba 2013

Ujumbe wa ngazi ya juu wa Umoja wa Ulaya umezomewa na wakaazi, wakati ulipotembelea kisiwa cha Lampedusa siku ya Jumatano, kufuatia ajali iliyowauwa watu wanaokaribia 300.

Rais wa Halamashuri ya Ulaya Jose Manuel Barroso akiwasili Lampedusa.
Rais wa Halamashuri ya Ulaya Jose Manuel Barroso akiwasili Lampedusa.Picha: picture-alliance/dpa

Ujumbe huo uliyokuwa unaongozwa na rais wa Halmshauri ya Ulaya Jose Manuel Barroso, ulimhusisha pia Kamishna wa umoja huo anaeshughulikia masuala ya ndani Ceclilia Malmostroem. Barosso ambaye aliahidi kiasi cha euro milioni 30 kwa serikali ya Italia kuisaidia kugharamia vituo vya wakimbizi wanaotafuta hifadhi, alisema maafa ya Lampedusa yameonyesha kuwa Ulaya haiwezi kuendelea kukaa kimya kuhusu tatizo la wahamiaji, na kwamba unapaswa kuongeza juhudi.

Wakati akizungumza, wapiga mbizi walikuwa wanaendelea na juhudi za kutafuta miili zaidi kutoka katika mabaki ya boti iliyokuwa imewabeba, ambayo ilishika moto na baadae kuzama umbali mdogo tu kutoka katika kisiwa cha Lampedusa. Kwa mujibu wa taarifa za sasa, watu 296 walifariki katika tukio hilo mbaya zaidi katika miaka ya hivi karibuni. Waokozi walifanikiwa kuwapata manusura 155 wa boti hiyo, ambayo inakadiriwa kuwa ilikuwa imebeba watu 500.

Kamishna Cecilia Malmostroem, rais Jose Manuel Barroso, na waziri mkuu Enrico Letta na waziri wake wa mambo ya ndani Angelino Alfano, wakiwa katika mkutano na waandishi wa habari.Picha: picture-alliance/dpa

Mateso na maumivu
Waziri mkuu wa Italia Enrico Letta, ambaye alimsindikiza Barroso, alisema Italia itafanya msiba wa kitaifa wa wahanga wa ajali hiyo, na itaongeza ufadhili kuwasaidia wahamiaji, wakiwemo watoto wengi wasiokuwa na wasimamizi.

Kikundi kidogo cha wahaharakati na wakaazi waliandamana kumpinga Barroso wakati akiwasili kisiwani hap. Baada ya maandamo hayo wajumbe hao wa Umoja wa Ulaya walitembelea kituo cha kupokea wahamiaji kilichojazana, kufuatia mabadiliko ya dakika za mwisho katika ratiba yao rasmi. Waziri mkuu Letta, alisema wakati akiondoka katika kituo hicho, kuwa ameona mateso na maumivu.

Wito wa kulegeza sheria za uhamiaji
Shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa lilisema jana kuwa mazingira ya kituo hicho, ambacho kina karibu watu 1,000 wakati uwezo wake ni watu 250 haikubaliki hata kidogo. Kamishna wa mambo ya ndani wa Umoja wa Ulaya, Cecilia Mamstroem alitoa wito kwa mataifa ya Ulaya kuimarisha wakala unaofanya doria doria mpakani wa Frontex, ili kuuwezesha kuendesha operesheni kubwa za uokozi katika bahari ya Mediterranean katika kipindi cha muda mfupi.

Manusura wa ajali hiyo akitembea katika mitaa ya Lampedusa Oktoba 8, 2013.Picha: Getty Images

Katika kipindi cha muda mrefu, alisema laazima kuwepo na hatua zaidi katika mataifa wanakotokea wahamiaji na wanakopitia, na pia kulegeza sheria kali za uhamiaji.

Kwa upande wake, rais wa Senegela Macky Sall, alisema kufunga mipaka, kuweka wakala wa Frontex na boti za doria ni njozi tu, kwa sababu watu wataendelea kuingia barani Ulaya, kwa sababu huo ndiyo mtirirko asili wa uhamiaji. Alisema kinachotakiwa ni kwa mataifa ya Ulaya kuja na sera za wazi zinazobainisha masharti nafuu kwa wanaotafuta kazi barnai humo, ili kuepusha maafa kama yaliyotokea.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/dpae,afpe.
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi