1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaLebanon

Joseph Aoun achaguliwa kuwa rais mpya wa Lebanon

9 Januari 2025

Bunge nchini Lebanon limepiga kura siku ya Alhamisi na kumuidhinisha kamanda wa jeshi Jenerali Joseph Aoun kuwa rais mpya wa taifa hilo.

Jenerali Joseph Aoun rais mpya wa Lebanon
Jenerali Joseph Aoun rais mpya wa LebanonPicha: Hussein Malla/AP/picture alliance

Katika jaribio la 13 la bunge kumchagua rais, Spika wa Bunge la Lebanon Nabih Berri amemtangaza Joseph Aoun kama rais mpya baada ya kupata ushindi kwa kura 99 kati ya 128 katika duru ya pili ya uchaguzi wa Bunge. Hapakuwa na matokeo yoyote baada ya duru ya kwanza iliyofanyika Alhamisi asubuhi.

Wakati akilihutubia Bunge baada ya kuidhinishwa, Aoun amesema nchi hiyo sasa inaingia katika enzi mpya. Amesema atachukua hatua zitakazohitajika ili kuhakikisha kuwa serikali yake ndio inakuwa na haki pekee ya kumiliki silaha.

"Ninaahidi kutekeleza jukumu langu kama Amiri Jeshi Mkuu na Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Ulinzi, ambapo nitafanya kazi kuthibitisha haki ya Serikali kuhodhi umiliki wa silaha."

Bunge la Lebanon likimuidhinisha Jenerali Joseph Aoun kama rais mpya wa LebanonPicha: Hussein Malla/AP/picture alliance

Kauli hiyo imeonekana kwa kiasi fulani kuilenga hifadhi ya silaha za kundi la Hezbollah  ambayo hapo awali hakuwahi kuizungumzia hadharani alipokuwa kamanda wa jeshi.

Joseph Aoun ambaye atatimiza umri wa miaka 61 kesho Ijumaa, ameapa kuwa ataheshimu na kudumisha makubaliano ya usitishaji mapigano na kumaliza ukaliaji wa Israel. Serikali mjini Tel-Aviv imesema ina matumaini kuwa rais huyo mpya wa Lebanon atasaidia kuleta hali ya utulivu.

Aoun aliyekuwa akiungwa mkono na Marekani na Saudi Arabia, anatazamwa kama kiongozi aliye katika nafasi nzuri zaidi ya kuikwamua pia nchi hiyo kutoka kwenye mzozo mkubwa wa kiuchumi na kifedha.

Aoun ashangiliwa ndani na nje ya Lebanon

Jenerali Joseph Aoun, rais mpya wa Lebanon akiwa kavalia sare za kijeshiPicha: Bilal Hussein/AP Photo/picture alliance

Wafuasi kadhaa wa Aoun walimiminika barabarani katika kijiji alichozaliwa cha Aishiyeh kusini mwa Lebanon ili kushangilia kuchaguliwa kwake. Wakaazi wa eneo hilo walikusanyika tangu asubuhi mbele ya kanisa ambalo lilikuwa limepambwa kwa bendera za Lebanon na picha yake.

Mataifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na Iran, Saudi Arabia, Ufaransa, Marekani, na Israel yamepongeza hatua hiyo na kutaja kuwa tayari kushirikiana na kiongozi huyo mpya.

Aoun ni kamanda wa tano wa jeshi la  Lebanon kuwa rais, akiwa pia ni wa nne mfululizo kushikilia wadhifa huo. Kulingana na mfumo wa dini nyingi kugawana madaraka nchini Lebanon, rais na wakuu wa jeshi wanatakiwa kuwa Wakristo wa madhehebu ya Wamaronite.

Aoun anakabiliwa na kibarua kigumu cha kusimamia usitishaji vita kwenye eneo la mpakani na Israel, kumteua waziri mkuu mpya atakayeongoza mageuzi yanayotakiwa na wakopeshaji wa kimataifa ili kuinusuru nchi hiyo kutoka katika mzozo mbaya zaidi wa kiuchumi katika historia yake.

(Vyanzo: AP, DPA, Reuters, AFP)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW