Joto jingi lazidi kuongezeka duniani: UN
23 Machi 2026
Shirika hilo limechapisha ripoti hiyo hii leo na limetahadharisha kwamba madhara ya ongezeko hilo la joto yatadumu kwa maelfu ya miaka ijayo.
Kulingana na ripoti hiyo, miaka 11 iliyopita kuanzia 2015 ndiyo 2025 ndiyo ilikuwa na viwango vya juu zaidi vya joto kuwahi shuhudiwa tangu mwaka 1850.
Likitoa ripoti hiyo ya kila mwaka, shirika la utabiri wa hali ya hewa ulimwenguni na tabia nchi la Umoja wa Mataifa (World Meteorologocal Organization) WMO limesema mwaka uliopita wa 2025 ulikiwa wa pili au wa tatu wenye joto zaidi kuwahi kurekodiwa.
Rekodi hiyo ikiwa ni takriban nyuzi joto 1.43 juu ya wastani ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kati ya 1850 hadi 1900.
Mwaka wa 2024 ndio ulikuwa wa joto zaidi kuwahi kurekodiwa, ukiwa na takriban nyuzi joto 1.55 juu ya wastani.
Guterres: Tabia nchi ipo katika hali ya dharura
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema tabia nchi ulimwenguni ipo katika hali ya dharura na kwamba sayari ya Dunia inasukumwa kupita mipaka yake. Kila kiashiria muhimu cha hali ya hewa kinaonyesha tahadhari kwa rangi nyekundu. Guterres amesisitiza kwamba wakati historia inapojirudia kwa miaka ya 11 mfululizo basi ni wito wa kuchukua hatua.
Ripoti ya Jumatatu inapaswa kuja na chapisho la tahadhari. Machafuko ya tabia nchi yanaongezaka kwa kasi na kuchelewa kuchukua hatua ni hatari maishani. Masuluhisho yetu lazima yajengwe kwenye msingi wa sayansi, busara na ujasiri wa kuchukua hatua
Mkuu wa shirika la WMO Celeste Saulo amesema mafanikio ya kisayansi yameboresha uelewa wa ukosefu huo wa usawa wa nishati na athari zake katika tabia nchi.
Hatua za binadamu zinazidi kuvuruga usawa wa hali asilia duniani na tutaendelea kukumbwa na madhara yake kwa mamia na maelfu ya miaka.
Ukosefu wa nishati inayoingia na inayotoka duniani
Kwa mara ya kwanza ripoti ya shirika la WMO imejumuisha ukosefu wa usawa wa nishati duniani- yaani kiwango ambacho nishati huingia na kutoka katika mfumo wa dunia.
Shirika hilo lenye makao yake makuu mjini Geneva limesema katika ukawaida wa hali ya hewa thabiti, nishati ya jua inayoingia duniani ni takriban sawa na kiasi cha nishati inayotoka.
Ukosofu huo wa usawa wa joto linaloingia na linalotoka kumeongezeka tangu kuanza kwa rekodi za uchunguzi mwaka 1960, hasa katika miaka 20 iliyopita. Kulifikia kiwango kipya cha juu mwaka 2025.
Joto jingi baharini
Zaidi ya asilimia 91 ya joto lililopitiliza huishia baharini. Kutokana na hiyo, viwango vya joto baharini vilikuwa juu zaidi mwaka 2025.
Shirika la WMO limesema joto baharini lina madhara mabayakama vile uharibifu wa mifumo ya ikolojia baharini, kupotea kwa bioanuwai na kupungua kwa uwezo wa bahari kufyonza kaboni.
Athari zaidi ni kwamba hali hiyo huchochea dhoruba za kitropiki na kuzidisha kutoweka kwa barafu baharini katika maeneo ya kaskazini mwa dunia, mfano Antaktika na Greenland.
Mwanasayansi wa WMO John Kennedy asema hali ya hewa ya dunia bado iko chini ya ushawishi wa La Nina, tukio la hali ya hewa linaloleta mabadiliko katika upepo, shinikizo la hewa na mifumo ya mvua.
(AFPE;RTRE)