1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Joto kuelekea mechi ya Yanga na Simba lazidi kutokota

23 Februari 2026

Mashabiki wa Simba wameanza kujinasibu kuwa safari hii ni ya kufuta uteja, wakikumbushia maumivu ya kupoteza michezo sita mfululizo dhidi ya watani wao wa jadi na mashabiki wa Yanga nao wanaonekana kujiamini.

Simba- Dar es Salaam - Tanzania
Mashabiki wa Simba ya Tanzania Picha: BackpagePix/empics/picture alliance

Wakati zikiwa zimesalia siku sita kufika Machi Mosi, siku ambayo macho na masikio ya wapenzi wa soka yataelekezwa visiwani Zanzibar kushuhudia Kariakoo Derby kati ya Yanga na Simba katika Dimba la New Amaan Complex, tambo za mashabiki zimeanza kupamba moto mapema.

Mashabiki wa Simba wameanza kujinasibu kuwa safari hii ni ya kufuta uteja, wakikumbushia maumivu ya kupoteza michezo sita mfululizo dhidi ya watani wao wa jadi.

“Itakuwa ni mechi ngumu sana, na Yanga sifikiri ataendeleza ule uteja kwa Simba Safari hii Simba wamejipanga,” alisema shabiki wa Simba, Lai Said.

Kwa upande wa Yanga mambo yakoje? Mashabiki wa Yanga wanaonekana kujiamini, wakiamini ubora wa kikosi chao na mwendelezo wa ushindi wa hivi karibuni utaendelea hata katika dabi hiyo.

“Mimi, kama shabiki wa Yanga Africans, jeuri tunaipata kwa sababu sisi tuna timu nzuri,” alisema shabiki wa Yanga, Magesa Mohamend.

“Atafungwa, na ndivyo ilivyo Timu yetu iko vizuri, imeimarika,” alisema shabiki mwingine wa Yanga.

Kikosi cha Yanga Picha: Mhindi Joseph

Nimezungumza na mchambuzi wa soka, Jacob Mlay, ambaye anaeleza kuwa licha ya takwimu na historia, Dabi ya Kariakoo hubeba sura yake ya kipekee.

“Maandalizi bora na utulivu kwenye mchezo huo vinaweza kuleta matokeo tofauti. Lakini tukiweka mbali takwimu za Yanga kushinda mechi nyingi, bado mechi itamuliwa zaidi na utulivu na maandalizi bora Timu zote zimefanya sajili, na Simba tumeona maongezeko yao kwenye kikosi Kwa hiyo, tunategemea mechi ngumu ya ushindani na derbi yenye sura ya kipekee kabisa,” alisema mchambuzi wa soka, Jacob Mlay.

Ligi kuu ya NBC inazidi kupamba moto.

Wakati presha ya dabi ikiendelea kupanda, Ligi Kuu Tanzania Bara nayo inaendelea kutifua vumbi. Jumatano, Simba watakuwa ugenini kukwaana na Dodoma Jiji FC.Simba wanaingia katika mchezo huo wakiwa na morali ya juu kufuatia ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Tanzania Prisons jana Jumapili. Mchezaji wa Simba, Seleman Mwalimu, anasema:

“Ni mchezo mgumu, lakini naamini tutarudi katika uwanja wa mazoezi tukiwa tayari Naamini mechi ya Dodoma jiji itakuwa nzuri Wakiwa nyumbani, wanakuwa wagumu.”

Mashabiki wa Yanga Picha: Mhindi Joseph

Kwa upande wa Yanga, wao walikusanya pointi tatu muhimu baada ya ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Namungo katika Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa, mkoani Lindi. Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves, anasema.

“Tulisema ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo kwamba tunahitaji kupigania na kuhakikisha tunapata pointi tatu kwa ajili ya watu wetu. Wanatusukuma sana na kutupa hamasa kubwa. Mwisho wa siku, ushindi ule ni kwa ajili yao. Tumefanikiwa kuupata ushindi huo,” alisema kocha wa Yanga, Pedro Goncalves.

Katika msimamo wa Ligi Kuu, JKT Tanzania wanaendelea kuongoza kwa alama 28 baada ya mechi 16 Yanga wanashika nafasi ya pili wakiwa na alama 25 baada ya mechi 9, huku Simba wakishika nafasi ya nne kwa alama 22 baada ya kucheza mechi 9.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW